Sunday, July 22, 2012

SMALLING APASULIWA MGUU, NJE WIKI 10

Chris Smalling

LONDON, Uingereza
BEKI wa Manchester United na timu ya taifa ya England, Chris Smalling huenda akawa nje ya uwanja kwa muda wa hadi wiki 10 baada ya kufanyiwa upasuaji wa mguu, kocha Alex Ferguson alisema jana Jumamosi.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22, ambaye hakusafiri na klabu kwenye ziara ya kujiandaa na msimu mpya nchini Afrika Kusini, alikosa mwisho wa msimu uliopita, na hakuitwa kwa ajili ya Euro 2012 na Olimpiki kutokana na majeraha ya nyonga.

Alitarajiwa kuwa tayari kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya England lakini akavunjika kidole gumba cha mguuni wakati wa mazoezi Jumatano, jambo linalomaanisha kwamba atakosa mwanzo wa msimu.

"Amepata majeraha Jumatano na moja kwa moja tukaamua afanyiwe upasuaji, hivyo hatakuwepo," Ferguson aliiambia televisheni ya klabu hiyo MUTV. "Ni ngumu kusema ni kwa muda gani atakuwa nje kutokana na majeraha yake lakini huenda ikawa wiki 10.

"Hana bahati hata kidogo huyu kijana, ni mdogo na tumefanya kila lililosahihi ili kumaliza tatizo lake haraka na kumrejesha kazini haraka iwezekanavyo."

Smalling anatarajiwa kuchuana na Nemanja Vidic, Jonny Evans, Rio Ferdinand na Phil Jones kuwania nafasi ya kuanza kama beki wa kati.

Nahodha wa Man United, Vidic anatarajiwa kuwa fiti kuanza msimu mpya baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti na kuwa nje kwa muda mrefu lakini Evans yuko shakani kucheza mechi ya ufunguzi wa ligi dhidi ya Everton Agosti 20 kutokana na matatizo ya 'enka'.

No comments:

Post a Comment