Tuesday, July 3, 2012

SERIKALI YAMPINGA SUGU UCHUNGUZI KUHUSU DK. ULIMBOKA

George Mkuchika

Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika, amesema kuwa serikali haioni sababu ya Bunge kuunda tume huru ya kuchunguza ukweli kuhusu unyama aliofanyiwa kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka kwa vile tayari suala hilo linashughulikiwa na vyombo husika.

Mkuchika alitoa maelezo hayo Bungeni mjini Dodoma leo wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge wakati wa kuhitimisha mjadala kuhusu makadirio na matumizi ya wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha.

Jana, mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini kupitia CHADEMA, Joseph Mbilinyi a.k.a Mr II Sugu,  alitaka iundwe tume huru ya kuchunguza ukweli kuhusu utekaji na unyama aliofanyiwa Dk. Ulimboka ambaye alikimbiziwa Afrika Kusini kuendelea na matibabu kwa vile Serikali haiaminiki kuhusiana na jambo hilo; huku pia akifananisha tukio hilo na unyama unaofanywa nchini Sudan na kikundi kinachotesa na kufanya mauaji dhidi ya wananchi cha ‘Janjaweed’.

Akiendelea kufafanua, Mkuchika alieleza kwamba Serikali inarudia tena kulaani tukio la kutekwa na kushambuliwa kwa Dk. Ulimboka, lakini akakana madai kuwa Serikali haiaminiki kama alivyosema Sugu kwavile matokeo ya uchaguzi mkuu uliopita (mwaka 2010) yalidhihirisha ni kwa kiasi gani serikali (ya CCM) inavyoaminika kwa wananchi.

Hivi karibuni, Dk. Ulimboka aliyekuwa miongoni mwa vinara wa mgomo wa madaktari alizua gumzo kubwa baada ya kukumbwa na tukio la kutekwa, kushambuliwa kinyama na kisha kutupwa kwenye msitu wa Mabwe Pande jijini Dar es Salaam. Hadi sasa haijajulikana wazi kuwa ni watu gani waliohusika na tukio hilo.

 

No comments:

Post a Comment