Tuesday, July 3, 2012

AVB ASAINI MIAKA MITATU KUIFUNDISHA TOTTENHAM

Kocha Andre-Villas Boas katika moja ya pozi zake maarufu awapo uwanjani.

LONDON, Uingereza
ANDRE Villas-Boas amesaini mkataba wa miaka mitatu ya kuifundisha Tottenham Hotspur, klabu hiyo ya Ligi Kuu ya England imetangaza leo.

Mreno huyo amechukua mikoba ya Harry Redknapp ambaye alitimuliwa Juni baada ya kuiongoza klabu hiyo ya White Hart Lane kwa miaka minne.

"Tottenham Hotspur ni klabu kubwa yenye utamaduni madhubuti na sapoti ya aina yake, kote nyumbani na dunia nzima. Naona upendeleo kuwa kocha hapa," Villas-Boas aliiambia tovuti ya Spurs (www.tottenhamhotspur.com).

"Hii ni moja ya nafasi bora za ukocha katika ligi kuu. Nimefanya majadiliano mengi na mwenyekiti (Daniel Levy) na bodi na najumuika nao katika mipango ya maendeleo ya klabu.

"Kikosi hiki kocha yeyote angependa kufanya kazi nacho na kwa pamoja naamini tunaweza kuleta mafanikio," Mreno huyo aliongeza.

Tottenham walimaliza katika nafasi ya nne kwenye ligi msimu uliopita chini ya Redknapp lakini walishindwa kufuzu kucheza Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kufuatia ubingwa wa Chelsea dhidi ya Bayern Munich katika fainali.

Villas-Boas, 34, alikuwa madarakani kwa miezi tisa tu Chelsea kabla ya kutimuliwa na mmiliki Mrusi Roman Abramovich mwezi Machi kufuatia mfululizo wa matokeo mabovu na ripoti za kukosekana utulivu katika chumba cha kuvalia.

Roberto Di Matteo alichukua madaraka Chelsea kama kocha wa muda na akaiongoza klabu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya na Kombe la FA.

Villas-Boas alipewa madaraka Stamford Bridge Juni 2011 kwa mkataba wa miaka mitatu na Chelsea wakalazimika kuilipa Porto paundi milioni 13.3 ili kumpata kocha huyo baada ya kuiongoza klabu hiyo kutwaa kombe la Ligi ya Europa na Ubingwa wa Ligi Kuu ya Ureno na Kombe la "FA".

No comments:

Post a Comment