Tuesday, July 24, 2012

SEEDORF AANZA NA KIPIGO BOTAFOGO

Mchezaji wa soka wa Uholanzi, Clarence Seedorf (kulia) akionyesha fulana iliyoandikwa "Seedorf, Carioca wa ukweli kuliko Waholanzi wote" huku Meya wa Rio de Janeiro, Eduardo Paes, akionyesha jezi ya Botafogo kabla ya mkutano wake wa kwanza na vyombo vya habari katika klabu yake mpya ya Botafogo katika jumba la Cidade Palace mjini Rio de Janeiro, Brazil Julai 9, 2012. Klabu ya Botafogo imemsajili Seedorf (36) kwa mkataba wa miaka miwili. Picha: REUTERS

KIUNGO wa zamani wa AC Milan, Inter Milan, Real Madrid na Ajax Amsterdam, Clarence Seedorf ameanza kucheza ligi kuu ya Brazil na kipigo baada ya klabu yake mpya Botafogo kulala 1-0 nyumbani dhidi ya Gremio.

Mholanzi huyo mwenye umri wa miaka 36, ambaye ameelezwa na rais wa Botafogo, Mauricio Assuncao kama mchezaji wa kigeni gwiji zaidi kupata kusajiliwa na timu hiyo ya Brazil, alicheza kwa kiwango cha chini, ingawa alipigiwa makofi na mashabiki wa nyumbani wakati akipumzishwa kuelekea mwishoni mwa mechi hiyo.

"Hali ya hewa ni nzuri, natumai kila mechi itakuwa hivi," aliwaambia waandishi wa habari baada ya mechi hiyo ya Jumapili.

"Seedorf amekuwa pamoja nasi kwa wiki mbili tu," alisema kocha Oswaldo de Oliveira. "Yeye ndio anaanza msimu wakati sisi tuko katikati."

Botafogo ni wa nane katika ligi hiyo yenye timu 20 kwa kuwa na pointi 17 kutokana na mechi 11.

No comments:

Post a Comment