Tuesday, July 24, 2012

PUYOL AREJEA BAADA YA KUPASULIWA GOTI

Carles Puyol

BARCELONA, Hispania
BEKI wa Barcelona, Carles Puyol amerejea mazoezini kwa mara ya kwanza tangu alipofanyiwa upasuaji wa goti mwezi Mei, klabu hiyo ya La Liga ilisema jana.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Hispania mwenye umri wa miaka 34 alifanyiwa upasuaji wa goti na akakaa nje katika wiki kadhaa za mwisho wa msimu, jambo lililomfanya akose ubingwa wa taifa lake wa Euro 2012 nchini Poland na Ukraine.

"Nahodha alifanya mazoezi mbali na wachezaji wenzake kabla hawajasafiri kwenda Ujerumani leo kwa ajili ya mechi yao ya kujiandaa na msimu mpya dhidi ya Hamburg," Barca ilisema katika tovuti yao (www.fcbarcelona.com).

"Puyol atafanyiwa uchunguzi mwingine wa kiafya Jumatatu ijayo, Julai 30, kuthibitisha uzima wake ili arejee kikamilifu mazoezini na wenzake - siku ambayo wachezaji wa kimataifa wa Hispania wataanza mazoezi," taarifa hiyo ilisema.

Mchezaji mwenzake Puyol, Dani Alves aliongeza katika mkutano na waandishi wa habari: "Nina furaha sana kwamba Puyi amerejea, kwamba yuko katika hali nzuri na anapona.

"Nadhani ukiwa na Puyi huhitaji kuangalia umri wake, kwa sababu haumaanishi chochote. Kwangu mimi, yeye ni kama mtoto wa miaka miwili."

No comments:

Post a Comment