Tuesday, July 24, 2012

SANAA KUTUMIKA MAONI YA KATIBA
KUTOKANA na kuonekana kwa matabaka miongoni mwa wananchi kuhusiana na uchangiaji wa maoni ya katiba, sasa sanaa pia itakuwa ni miongoni mwa nyenzo zitakazotumika katika uchangiaji wa maoni hayo nchini.

Chama cha wanafunzi waliofadhiliwa na shirika la Ford Foundation ndicho kitakachosimamia mchakato huo wa kutumika kwa sanaa katika kutoa maoni hayo.

Tayari mwishoni mwa wiki iliyopita tamasha moja limefanyika kama uzinduzi huku likionekana kuvuta hisia za watu wengi ambao walielimishwa kupitia maigizo na sanaa ya uimbaji na kuonekana kwa kiasi fulani kuelewa kinachoongelewa na kupata fursa ya kutoa maoni yao.

Matamasha hayo ya uhamasishaji wa wananchi kwa ajili ya kutoa maoni kuhusu Katiba Mpya, yalizinduliwa katika Viwanja vya Mburahati kwa Jongo, na kuhudhuriwa na umati wa wakazi wa wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Tamasha hilo ni mfululizo wa matamasha mengi ambayo yatakuwa ni maalum kwa ajili ya wananchi kupata fursa ya kutambua haki zao kwa kupitia burudani.

Akizungumza Dar es Salaam juzi, Kiongozi wa Chama Cha Wanafunzi waliofadhiliwa na Shirika la Ford Foundation la Marekani, Harold Sungusia alisema kuwa wameamua kuzindua tamasha hili Dar es Salaam kwa ajili ya kuhamamsisha jamii ipate kujua haki zao kwa kupitia burudani mbalimbali.

Alisema kuwa baada ya uzinduzi wa tamasha hilo, pia wanaandaa tamasha lingine ambalo litafanyika katika Viwanja vya Biafra Dar es Salaam na baadaye kulipeleka mikoa yote ya Tanzania bara.

Alisema kuwa sanaa wanazotumia kufikisha ujumbe kwa jamii ni pamoja na ngoma, maigizo, tamthilia na sarakasi.

Alisema kuwa watakuwa wanatumia mfumo wa burudani mbalimbali kwa ajili ya kuwakusanya watu zaidi na kuwapatia elimu kwa kupitia burudani hizo.

Alisema kuwa lengo lao ni kutoa elimu ya kwa jamii kwa ajili ya kutoa maoni juu ya Katiba mpya ambapo wao wameamua kuanzia ngazi za chini kutokana na watu wengi 
kutokuwa na uelewa mzuri juu ya Katiba Mpya.

"Tumeamua kuzindua tamasha hili ambalo litakuwa linaendeshwa na burudani kwa asilimia kubwa ambapo lengo letu ni kutoa elimu kwa jamii juu ya kutoa maoni kuhusu Katiba Mpya," alisema.

Katika tamasha hilo Mgeni Rasmi alikuwa Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda ambaye alisema kuwa watu wengi hawajui maana ya Katiba hivyo wanashindwa kutambua haki zao.

Alisema kuwa kupitia tamasha hili ambalo litafanyika pia kila mkoa, watu watapata fursa ya kutambua haki zao za msingi.

No comments:

Post a Comment