Tuesday, July 31, 2012

REAL YAKATAA KUMTOA KAKA KWA MKOPO

Kaka

MADRID, Hispania
REAL Madrid haina mpango wa kumruhusu Kaka kujiunga na AC Milan kwa mkopo wa mwaka mmoja na badala yake wanataka kumuuza jumla, gazeti la Marca limeripoti.
Milan ambao ni vigogo wa Serie A, Ligi Kuu ya Italia wamepania kumrejesha kiungo huyo nyota wa kimataifa wa Brazil katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi, na tayari wameshazungumza na wakala wa mchezaji huyo kujadili uwezekano wa kumsajili.
Hata hivyo, hali ngumu ya kifedha waliyo nayo Milan inakwaza dhamira yao, na klabu hiyo ina matumaini ya kumsajili Kaka kwa mkopo bila kulipia ada ya uhamisho, huku pia wakiiomba Real kuendelea kumlipa asilimia 50 ya mshahara wa kiungo huyo.
Real hawautaki mpango huo na badala yake wako tayari kumruhusu aondoke kwa mkataba wa kudumu.
Mazungumzo baina ya klabu hizo yataendelea katika siku zijazo, na Real ambao ni mabingwa wa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania, watasisitiza kwamba Milan ni lazima waonyeshe dhamira ya kweli ya kumhitaji Kaka kabla ya kuendelea na majadiliano yao.



No comments:

Post a Comment