Wednesday, August 1, 2012

MWANDOSYA: NILIMUOMBA MUNGU ANIPE JAPO DAKIKA 5 NIJE KUSHUKURU BUNGENI

Prof. Mark Mwandosya

Aisee angalia usije ukateleza...! Rais Jakaya Kikwete akitaniana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Prof. Mark Mwandosya

WAZIRI wa Nchi katika Ofisi ya Rais Asiye na Wizara Maalum, Profesa Mark Mwandosya, amerejea bungeni kwa mara ya kwanza leo katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja kutokana na matatizo ya kuugua yaliyomfanya atumie kipindi chote hicho katika matibabu, yakiwamo aliyoenda kuyapata nchini India.

Profesa Mwandosya aliutumia muda wake wa kuzungumza bungeni kuwashukuru wabunge, Watanzania na wote walioshiriki kumsaidia na kumuombea katika kipindi kigumu cha ugonjwa.

"Ukiugua kumbe kunakuwa hamna chama. Tofauti zote za kiitikadi zinawekwa pembeni watu wanaungana kwa ajili ya kukuombea bila ya kujali ni chama gani," alisema.

"Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kuwa hapa leo. Nawashukuru wote kwa sapoti yenu. Namshukuru pia Rais Jakaya Kikwete, alinisisitiza kwamba afya kwanza. Aliniambia usifikirie kwamba sijui kuna kijiji fulani hakina maji. Shughulikia afya yako kwanza. Na kweli, ona sasa mimi si Waziri wa Maji tena.

"Kwa hakika nilikuwa katika kipindi kigumu. Nilimuomba Mungu anipe japo dakika tano nije nizungumze tena hapa (bungeni) na wenzangu.

"Napenda kuwasisitiza kwamba daima tupime afya zetu. Mimi nilikuwa sijakiona kitanda (kulazwa kwa ugonjwa) kwa miaka 45. Nilidhani mimi ni mzima sana kwa sababu nafanya mazoezi kila siku, lakini kumbe bado ni binadamu tu na Mungu ana mipango yake. Tupime afya kila mara," alisisitiza Mwandosya katika muda wake wa kuzungumza ambao aliutumia wote kutoa shukurani zake.

"Katika kipindi chote hicho, nimebaini kuwa kumbe kwenye kuumwa hakuna siasa... watu wengi walinijulia hali na kunitakia uzima bila kujali kuwa ni wa CCM, Chadema, TLP na vyama vingine," aliongeza Prof. Mwandosya.

Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni leo, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Mbunge wa Kigoma Kaskazini,
Mhe. Zitto Kabwe, alisimama na kusema wao kama kambi ya upinzani wanamtakia afya njema Profesa Mwandosya na wanamkaribisha kwa mikono miwili.

No comments:

Post a Comment