Tuesday, July 24, 2012

SUGU ATAKA MIKATABA BORA YA AJIRA KWA KINA JULIO, MKWASA

Mhe. Sugu akifanya vitu vyake bungeni

Kocha Jamhuri Kihwelu 'Julio' akiwajibika wakati akiifundisha timu ya taifa ya vijana wa Tanzania wenye umri wa chini ya miaka 23.
Kocha Charles Boniface Mkwasa akiwa kibaruani wakati akiiongoza timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars.
 Mbunge wa Mbeya Mjini (CHADEMA), Mhe. Joseph Mbilinyi ‘Mr. II-Sugu’ ameitaka serikali itekeleze mara moja ahadi yake ya kuhakikisha kwamba makocha wazawa wanaandaliwa mikataba yao ya ajira ili nao walipwe vizuri na kwa uhakika tofauti na ilivyo sasa ambapo wageni pekee ndio hufaidika kwa kulipwa mamilioni ya pesa.

Mhe. Sugu ameyasema hayo mchana huu wakati akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa mwaka ujao wa fedha.

Sugu ambaye pia ni Waziri Kivuli wa wizara hiyo, alisema kuwa inasikitisha kuona kuwa makocha wazawa (kama Jamhuri Kihwelu ‘Julio’,  Boniface Mkwasa, Juma Pondamali) wakikosa mikataba itakayowahakikishia maslahi bora huku wageni wamekuwa wakilipwa fedha nyingi; ambapo hata katika bajeti ya sasa, imeonyesha kuwa zimetengwa jumla ya Sh. milioni 400 kwa ajili tu ya kuwalipa mishahara makocha wa kigeni.

Alikumbushia kuwa katika bajeti iliyopita, aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Dk. Emmanuel Nchimbi, aliahidi kutekeleza ushauri wa kambi ya upinzani kuhusiana na suala hilo na kwamba, tayari Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeanza mchakato wa kuandaa mikataba ya makocha wazawa.

“Je, utekelezaji wa suala hili umefikia wapi?” alihoji Sugu.

No comments:

Post a Comment