Saturday, July 7, 2012

NANI AZIDI KUMKAANGA CRISTIANO RONALDO


Wachezaji wa Ureno wakiwa viroho juu wakati wa hatua ya 'matuta' dhidi ya Hispania katika nusu fainali ya Euro 2012. Nani yuko kushoto, Ronaldo kulia.
Nani (kushoto) na Ronaldo wa Ureno wakishangilia katika mechi mojawapo ya fainali za Euro 2012 

PORTO, Ureno
WINGA Luis Nani wa timu ya taifa ya Ureno amefichua kwa mara nyingine kwamba nahodha wake Cristiano Ronaldo aling’ang’ania kupiga penati ya mwisho wakati wa hatua ya ‘matuta’ ya mechi yao ya nusu fainali ya Euro 2012 dhidi ya Hispania.

Kutokana na kukosa kwa Joao Moutinho na Bruno Alves, nyota huyo wa Real Madrid alikoseshwa nafasi ya kupiga penati yake, ambayo pengine ingewavusha kwa hatua ya fainali baada ya goli alilofunga Cesc Fabregas kuwahakikishia Hispania ushindi wa penati 4-2.

Nani ambaye pia ni winga wa Manchester United, amesema kwamba hakukuwa na utata wowote kuhusiana na uchaguzi wa watu wa kutangulia kupiga penati, lakini aliongeza kwamba Ronaldo alitaka apige penati ya tano.

“Sidhani kama kulikuwa na tatizo au makosa yoyote yaliyofanyika,” winga huyo mwenye miaka 25 aliliambia gazeti la Times of India.
“Cristiano alitaka kupiga penati ya mwisho. Nilimwambia kocha niko tayari kupiga penati yoyote ile. Kwangu sikuona kama kuna tatizo kwa sababu mikwaju ya penati huwa inategemea bahati na kwakweli hatukustahili kutolewa kivile.”

Licha ya kuondolewa katika nusu fainali hiyo, Nani anaamini kwamba kikosi chao kilichoongozwa na kocha Paulo Bento kinastahili kujivunia kiwango walichoonyesha katika fainali za Euro 2012 zilizofanyika katika nchi za Poland na Ukraine.

“Ni wazi kwamba tuliondoka tukiwa na huzuni tele baada ya kutolewa kwa sababu tulikaribia kufika fainali, hata hivyo tunaweza kujifariji kutokana na kile tulichokifanya.

“Tulijitolea kadri ya uwezo wetu wote. Tulionyesha kiwango cha juu. Mwishowe Hispania walikuwa na bahati zaidi kulinganisha na sisi kwa sababu kila zinapopigwa penati, bahati ndio huamua mshindi.

“Wao ni mabingwa waliostahili, lakini nadhani kwamba katika nusu fainali yetu tulistahili kuwafunga. Kwahiyo watu wa Ureno wanaweza kujivunia timu yao. Tuna huzuni kwa sababu tulistahili kutinga fainali, hata hivyo tulirudi nyumbani  huku vichwa vyetu vikiwa juu,” alihitimisha.

Hispania ambao pia ni mabingwa wa Dunia, waliendeleza moto wao kwa kuwashindilia Italia mabao 4-0 katika mechi yao ya fainali na kuatwaa ubingwa wa tatu mfululizo katika michuano ya kimataifa.

No comments:

Post a Comment