Saturday, July 7, 2012

VALDES: MAKIPA TUTAPATA HESHIMA CASILLAS AKITWAA TUZO YA FIFA BALLON D'OR

Muwe mdaka hivi...! Kipa Iker Casillas akijifua na Valdes (kulia) na Pepe Reina wa timu ya taifa ya Hispania.

Usafiri wa 'pipa' mtamu sana... hapa Valdes akiwa ndani ya ndege na wachezaji wenzake wa Hispania, Iniesta (kulia) na Sergio Busquet

Valdes akishikilia kombe walilotwaa la Euro 2012

MADRID, Hispania
Kipa wa klabu ya Barcelona, Victor Valdes amesema kuwa, ikiwa Iker Casillas wa mahasimu wao wa jadi, Real Madrid atatwaa tuzo ya FIFA ya Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Dunia (Fifa Ballon d'Or) itakuwa ni heshima kubwa kwa makipa.

Hasimu huyo wa Casillas katika mechi zao za watani wa jadi maarufu kama ‘el clasico’, aliweka kando upinzani wao wakati wote wawili walipokuwa wakiitumikia timu ya taifa lao la Hispania iliyotwaa ubingwa wa Euro 2012.

Baada ya Casillas ambaye ni nahodha kuiongoza vyema Hispania katika fainali za Euro zilizoandaliwa na nchi za Poland na Ukraine, kipa huyo wa Real Madrid amekuwa akitajwa na baadhi ya wataalam wa soka kuwa ndiye anayestahili kuwa mshindi wa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Dunia, jambo ambalo Valdes anaamini kwamba ni sahihi kama kweli litatokea.

“Itakuwa heshima kubwa kuwa na kipa mshindi wa tuzo ya Ballon d’Or,” tkipa huyo wa Barca aliviambia vyombo vya habari vya Hispania. “Hata hivyo kuna wachezaji wengine ambao pia wanaweza kushinda tuzo hii. (Andres) Iniesta namkubali sana na nimefurahi sana kwa kutambuliwa na kupewa tuzo alizo nazo."

HISPANIA = BARCELONA
Valdes aliendelea kueleza kwamba mtindo wa kucheza wa Hispania ulifanana na Barcelona, na pia akatoa kauli ya kumuunga mkono kocha mpya wa Barca, Tito Vilanova.

Tito Vilanova
“Nadhani falsafa ya mchezo wa Barcelona imekuwa ya kuvutia kwa miaka kadhaa, na sasa Hispania inacheza kwa mtindo huohuo. Ni kawaida kwa sababu wachezaji wengi wa Barcelona pia wanaichezea Hispania.

“Chini ya Vilanova hakutakuwa na mabadiliko makubwa. Ni wakati wa kuwa makini na kutambua kwamba baada ya (Pep) Guardiola kuna hatua nyingine. Namuamini sana kwa sababu namjua vizuri kocha Tito,” alisema.

NEYMAR
Neymar wa Brazil (kushoto) akituliza mpira mbele ya Lionel Messi wa Argentina katika mechi yao ya hivi kirafiki hivi karibuni. Valdes anakiri kwamba Neymar ana kipaji cha aina yake na kwamba, ni lazima kila timu itamtaka tu.
Mwishowe, Valdes pia alimzungumzia straika yosso mwenye kipaji wa Brazil, Neymar, ambaye siku za nyuma alikuwa akihusishwa na uhamisho wa kwenda klabu za Barcelona na Real Madrid.

"Neymar ana kipaji cha ajabu. Anafanya vitu ambavyo ni vigumu kuiga. Ni mchezaji ambaye timu yoyote ile itamtaka tu,” alihitimisha Valdes.

No comments:

Post a Comment