Saturday, July 7, 2012

ARUSHA NI BALAA EPIQ BSS

Mkurugenzi wa Masoko wa Zantel Deepak Gupta akiimba pamoja na washiriki waliojitokeza kuwania nafasi ya kuchaguliwa kuwakilisha mkoa wa Arusha katika ngazi ya taifa ya shindano la EBSS.
Majaji wa EBSS 2012 wakifuatilia kwa makini washiriki waliokuwa wakiimba.


Na Mwandishi Wetu, Arusha
VIJANA wa mkoa wa Arusha wanafahamika kwa jinsi wanavyoupenda muziki wa hip hop na mtaani huuponda sana muziki wa kuimba.

Lakini katika kuthibitisha kuwa dunia inageuka, kwenye usaili wa shindano la kusaka vipaji vya kuimba la Epiq Bongo Star Search 2012, vijana wengi wameamua kuimba hali iliyowafurahisha majaji wa shindano hilo.

Umati mkubwa wa wasichana na wavulana wakiwa na vyombo mbalimbali vya muziki walifurika katika ukumbi wa Triple A jijini hapa kwa ajili ya kugombea kuchaguliwa kuiwakilisha Arusha katika shindano hilo linalochukua waimbaji watano toka kila mkoa.

Akizungumzia mwamko huo, Jaji Mkuu wa EBSS 2012, Ritha Paulsen aliwaambia waandishi wa habari mkoani hapa kuwa kadri muda unavyoenda amekuwa akipata wakati mgumu kuchagua mwakilishi wa mkoa huu katika ngazi ya taifa.

Alisema kuwa tofauti na mikoa mingine ambapo ilikuwa ikiwachukua muda mrefu kuona vipaji lakini kwa Arusha ameviona vipaji ndani ya dakika thelathini za mwanzo.

"Mimi nadhani hii inatokana na ukweli kwamba Arusha ni jiji na inaonekana kuwa watu wa hapa walijipanga kwelikweli kwa kuwa takriban kila anayekuja kuimba ni mkali," alisema Ritha.

Jaji mwingine Master Jay alikiri kuwa inatakiwa badala ya kuchukua washiriki watano kwa mkoa huu ni bora hata ikaongezwa idadi kwa kuwa waliojitokeza wengi wana vipaji.

"Mimi nilikuwa nadhani kwa kuwa huu ni mkoa wa wapenda muziki wa Hip Hop lakini nimeona kuwa kwa mwaka huu watu wamebadilika kweli kweli wameimba na wamejipanga vema,” alisema Master Jay.

Kama ilivyokuwa kwa mikoa mingine, mkoa wa Arusha nao pia kulikuwa na zoezi la uchangiaji damu, ambapo Mkurugenzi wa Masoko wa Zantel, Deepak Gupta alisema kuwa kampuni hiyo ya huduma za simu mbali na kutambua umuhimu wa ajira kwa vijana lakini pia inawatengenezea mtandao wa kujihusisha na masuala ya kijamii kama hilo la kuchangia damu.

"Zantel ni kampuni ambayo inamilikiwa na wazawa, na hivyo jamii ndio kipaumbele chetu katika kila jambo. Hapa Arusha kama ilivyo mikoa mingine, tumechangia damu, lakini pia tumewawezesha kimawasiliano madiwani wa jiji la Arusha kwa kuwapa simu za mikononi," alisisitiza bwana Gupta.


------------

No comments:

Post a Comment