Saturday, July 7, 2012

KALOU APIMA AFYA LILLE, APEWA MIAKA MINNE

Siamini, yaani Chelsea wameona sifai?........... Salomon Kalou wakati akiwa Chelsea kabla ya kutemwa

STRAIKA wa zamani wa Chelsea, Salomon Kalou anajiandaa kwenda kufanya vipimo vya afya kabla ya kusaini mkataba wa miaka minne na klabu ya Lille ta Ligi Kuu ya Ufaransa wikiendi hii, gazeti la La Voix du Nord limeripoti.
   
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ivory Coast aliripotiwa kuwasili katika mji huo uliopo kaskazini Ufaransa akiwa na kaka yake ambaye pia ni ndiye mshauri wake na nahodha wa zamani timu yao ya taifa, Bonaventure Kalou, kuelekea kufanyiwa vipimo hivyo leo jioni baada ya klabu hiyo kuonekana imeshinda mbio za kuwania kumsajili straika huyo wa aliyekuwa akitakiwa na klabu 12 kubwa za Ulaya.

Kalou (26) anaaminika kujadili masuala ya soka na fedha pamoja na bonasi ya kusaini mkataba na Lille, na atamwaga wino mara atakapoidhinishwa na timu ya madaktari wa mabingwa hao wa Ufaransa.

Straika huyo alicheza miaka sita Stamford Bridge, akifunga magoli 60 katika mechi 244 za kimashindano akiwa na klabu hiyo, lakini alijikuta akikosa nafasi ya kutosha kucheza msimu uliopita, akipangwa mara 12 tu katika Ligi Kuu ya England kabla ya kutemwa na mabingwa hao wa Ulaya mwezi uliopita.

Kalou anatarajiwa kuwa mchezaji wa nne kujiunga na Lille katika kipindi hiki cha usajili, kufuatia kutua kwa Marvin Martin, Steeve Elana na Viktor Klonaridis.

No comments:

Post a Comment