Tuesday, July 24, 2012

MOURINHO ASHINDA BONGE LA TUZO URENO


Jose Mourinho akishangilia baada ya kutwaa taji la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya wakati akiifundisha Inter Milan ya Italia.
LISBON, Ureno
KOCHA wa Real Madrid, Jose Mourinho atapokea tuzo ya Fernando Soromenho Ijumaa ambayo hutolewa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Ureno (CNID) kutokana na mafanikio yake katika mchezo wa soka.

Kocha huyo mwenye miaka 49, atakabidhiwa tuzo hiyo kwenye hoteli ya Pestana Palace mjini Lisbon, na baada ya hapo atazungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari.

Hiyo ni tuzo inayopewa heshima ya juu zaidi kutoka CNID, ambayo ilianzishwa mwaka 1967.

Mourinho, aliyeanza kazi ya ukocha mwaka 2000 katika klabu ya Benfica, aliisaidia Porto kutwaa taji moja la Kombe la UEFA na kombe jingine la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya katika kipindi cha miaka miwili ya kuiongoza klabu hiyo.

Akaendeleza moto wake kwa kutwaa mataji kadhaa baada ya kuhamia Chelsea na Inter Milan kabla ya kutua Real Madrid wakati wa usajili wa majira ya kiangazi mwaka 2010. Hadi sasa, tayari ameshaipa Real Madrid Kombe la Mfalme (Copa del Rey) na jubingwa wa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania.

No comments:

Post a Comment