Tuesday, July 24, 2012

KOSCIELNY AJIFUNGA MIAKA MINGI ARSENAL

Laurent Koscielny

BEKI wa kimataifa wa Ufaransa, Laurent Koscielny amesaini mkataba mpya wa muda mrefu na Arsenal, klabu hiyo ya Ligi Kuu ya England imetangaza leo.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 amekuwa nguzo muhimu ya ulinzi ya kikosi cha kocha Arsene Wenger na kiwango cha juu alichoonyesha katika ligi hiyo ya juu Uingereza kimempatia nafasi ya kuichezea timu yake ya taifa ya Ufaransa mara 4 ikiwemo kuitwa katika kikosi kilichoenda kwenye fainali za Euro 2012.

"Laurent amekuwa katika kiwango bora pamoja nasi kwa misimu miwili iliyopita," Wenger aliiambia tovuti ya klabu hiyo (www.arsenal.com).

"Unapozingatia hilo tangu 2009 alipokuwa akicheza katika daraja la kwanza Ufaransa (Ligue 2) na kwamba hivi sasa anacheza kwa kiwango cha juu katika Ligi Kuu ya England na timu yake ya taifa, maendeleo aliyoonyesha ni ya kipekee kabisa.

"Laurent ni mchezaji wa kiwango cha juu na nina furaha sana ameamua kujifunga kwenye klabu."

Koscielny aliisaidia Arsenal kufuzu kucheza Ligi ya Klabu Bingwa 2012/13 wakati alipofunga goli la ushindi dhidi ya West Bromwich Albion katika siku ya mwisho wa msimu.

Alisema amefurahia kuongeza mkataba huo na anatarajia makubwa ya baadaye akiwa na Gunners.

"Nina furaha kufikia muafaka na klabu. Nimekuwa na kipindi kizuri hapa na natarajia mafanikio makubwa ya baadaye na Arsenal," alisema Koscielny.

Beki huyo wa kati alijiunga na Arsenal akitokea katika klabu ya FC Lorient mwaka 2010 na baada ya majeraha kumharibia mwanzo wake, ameibuka na kucheza jumla ya mechi 85 akiwa na Arsenal.

No comments:

Post a Comment