Tuesday, July 24, 2012

MIILI MINGINE 21 YA BOTI ILIYOZAMA YA MV SKAGIT YAOPOLEWA BAHARINI LEO, SASA MAITI ZAFIKIA 98


Wananchi wakiendelea na zoezi la uopoaji maiti za ajali ya kuzama kwa Mv Skagit.
Maiti zaidi wakiteremshwa baada ya kuopolewa baharini.

Askari waliokuwa wakishughulikia zoezi la kusaka miili ya watu waliokufa katika ajali ya Mv Skagit wakiwa katika eneo la Bandari ya Zanzibar kabla zoezi hilo kusimamishwa awali. (Picha: Ramadhan Othman - Ikulu)

Miili mingine 21 ya watu waliozama na boti ya Mv Skagit iliyokuwa ikisafiri kutoka jijini Dar es Salaam kuelekea Zanzibar imepatikana leo na hivyo kuongeza idadi ya maiti wote waliopatikana kufikia 98.


Taarifa zilizothibitishwa na Polisi Zanzibar jioni hii zimeeleza kuwa miili hiyo imepatikana katika maeneo mbalimbali, yakiwamo ya Chumbe kulikotokea ajali hiyo, Pume na Punguja.


Jeshi hilo limesema kuwa miongoni mwa miili iliyopatikana, umo wa mgeni mmoja kutoka Uholanzi na kwamba.

Licha ya awali kutangazwa na Serikali juu ya kusitishwa rasmi kwa zoezi la kutafuta miili zaidi, bado juhudi zimekuwa zikiendelea kufanywa na serikali kwa kushirikiana na wananchi katika kusaka miili ya watu waliokufa kutokana na ajali hiyo.


Wakati ikizama katika eneo la Chumbe, boti hiyo ilikuwa na watu zaidi ya 340. Inahofiwa kuwa baadhi ya miili ya waliokufa bado imenasia ndani ya boti hiyo ambayo imezama chini kabisa mwa kina kirefu cha bahari kinachokadiriwa kuwa ni cha zaidi ya mita 60.


Boti ya Mv Skagit ilikumbwa na ajali hiyo Julai 19 wakati ikiwa katika eneo la Chumbe. Ilidaiwa kwamba awali ilipigwa na dhoruba kali mishale ya saa 7:00 mchana, ikapinduka na kisha boti hiyo ndipo ikazama yote baharini.

No comments:

Post a Comment