Monday, July 30, 2012

MGOMO WA WALIMU WAZUA BALAA MBEYA, WANAFUNZI WAJILAZA BARABARANI KUUNGA MKONO WALIMU WAO, OFISI YACHOMWA, POLISI WADHIBITI VURUGU


Kamanda wa Polisi Mkoani Mbeya, Diwani Athumani

Mbunge wa Mbozi Magharibi, Mhe. David Silinde
Rais wa CWT, Gratian Mukoba

Naibu Waziri wa Elimu, Mhe. Phillip Mulugo.
Mgomo wa walimu nchini kote ulioanza leo umezua kizaazaa katika mji mdogo wa Tunduma mkoani Mbeya baada ya wanafunzi wa baadhi ya shule kujilaza barabarani katika kile walichodai kuwa ni kuishinikiza serikali isikilize madai ya walimu na hivyo kuwapa fursa ya kuendelea na masomo.

Akizungumza bungeni mchana huu wakati akiomba mwongozo wa Naibu Spika kwa kutumia kifungu cha 68 cha kanuni za Bunge, Mbunge wa Mbozi Magharibi (CHADEMA), Mhe. David Silinde, alisema kuwa magari yalikuwa yakishindwa kupita katika barabara kuu inayoelekea Zambia kutokana na vurugu zilizosababishwa na mgomo huo wa walimu ulioungwa mkono na wanafunzi na kwamba hadi wakati akitpa taarifa hizo, tayari kuna ofisi ya halmashauri imeshachomwa moto.

Silinde akaeleza zaidi kwamba Polisi wameshafika eneo hilo na vurugu zilikuwa zikikwamisha shughuli mbalimbali za kila siku.

Mbunge huyo akamuomba Naibu Spika atoe mwongozo wake kuhusiana na mgomo wa walimu kwani ijapokuwa wanazuiwa wasijadili suala hilo kwa maelezo kuwa liko mahakamani, anadhani kwamba kuna haja ya kiti cha spika kutafuta namna ya kulishughulikia kwa dharura suala hilo bila kuingilia mhimili wa mahakama kwani linawaathiri wananchi wa kawaida.

Akitoa maelezo yake baada ya kuombwa mwongozo na Silinde, Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai, aliwataka wabunge wampe muda hadi jioni ili atoe mwongozo wake kuhusiana na jambo hilo, na mambo mengine mawili aliyoombwa na waheshimiwa Kangi Lugora na James Mbatia (kuhusu suala la umeme) na John Mnyika aliyeomba mwongozo juu ya kufikishwa bungeni kwa taarifa ya kamati ya kudumu ya bunge ya huduma za jamii kuhusiana na mgomo wa madaktari.

Wakati huo huo, Kamanda wa Polisi Mkoani Mbeya, Diwani Athumani, amekiri kutokea kwa vurugu hizo na kusema kwamba hali sasa inaendelea kuwa shwari baada ya jeshi lake kufanikiwa kuwatawanya wanafunzi waliokuwa wamejilaza barabarani.

Akizungumza mchana huu kupitia mahojiano yake na Televisheni ya Taifa (TBC1), Kamanda Athumani aliwataka wananchi kuwa watulivu na kujiepusha na vitendo vya vurugu kwani vinarudisha nyuma shughuli za maendeleo.

Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kupitia rais wake, Gratian Mukoba kilitangaza kuanza kwa mgomo wa walimu nchini kote kuanzia leo ili kushinikiza madai ya stahili zao mbalimbali.

Hata hivyo, serikali kupitia Naibu Waziri wa Elimu, Phillip Mulugo, iliwaonya walimu kujiepusha na mgomo huo kwani si halali na kwamba suala hilo liko mahakamani.

No comments:

Post a Comment