Monday, July 30, 2012

GAZETI LA MWANAHALISI LAFUNGIWA KWA MUDA USIOJULIKANA

Moja kati ya 'stori' kubwa zilizoongoza matoleo ya hivi karibuni ya gazeti la Mwanahalisi.

Sehemu ya ukurasa wa mbele wa toleo la hivi karibuni la gazeti la Mwanahalisi
Gazeti la kila wiki la Mwanahalisi limefungiwa kwa muda usiojulikana kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kuandika habari na makala za uchochezi.

Sababu nyingine ya kufungiwa kwa Mwanahalisi imeelezwa kuwa ni pamoja na habari na makala zake kujenga uhasama na uzushi likiwa na nia ya kusababisha wananchi kukosa imani na vyombo vya dola, hali inayoweza kuhatarisha amani na mshikamano wa nchi.


Akisoma tamko la serikali leo jijini Dar es salaam, Kaimu Mkurugenzi Wizara ya Habari (MAELEZO), Phabian Lugaikamu, alisema kuwa matoleo ya Mwanahalisi, namba 302, 303 na 304 ya mwaka 2012 na mengine yaliyotangulia, yalichapisha habari na makala zenye kueneza na kujenga hofu kwa jamii.

"Mhariri wa gazeti la Mwanahalisi ameitwa na kuonywa mara nyingi lakini hataki kukiri kuwa maudhui ya makala zake hayana tija kwa jamii, pia hazifuati weledi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari," alisema

Aidha alisema kuwa mhariri huyo mara zote katika utetezi wake amekuwa akinukuu kifungu cha 18 cha katiba ya nchi kinachotoa uhuru wa kutoa maoni na kwa makusudi kutokunukuu kifungu ca 30 cha katiba hiyo kinachoweka ukomo wa uhuru.
  
"Serikali imeamua kulifungia gazeti hilo kutochapishwa kwa muda usiojulika kwa mujibu wa sheria ya magazeti ya mwaka 1976, kifungu namba 25(i), adhabu hiyo itaanza tarehe 30 Julai, 2012 kwa mujibu wa tangazo la serikali namba 258 lililochapishwa katika gazeti la Serikali na kutolewa jijini Dra es salaam Julai 27,2012," alisema.

ALIYEMTEKA DK. ULIMBOKA

Uamuzi huu wa kulifungia Mwanahalisi umekuja ikiwa ni siku chache  tu baada ya gazeti hilo kuwatuhumu na kuwataja kwa majina baadhi ya maafisa wa Idara ya Usalama wa Taifa kuwa ndio waliohusika na tukio la kumteka kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, kwa habari iliyokuwa na kichwa cha habari kinachosema: "Aliyeteka Ulimboka huyu hapa".

Hivi karibuni, gazeti hilo pia lilichapisha taarifa zilizowahusisha watu wa Usalama wa Taifa kwa habari iliyokuwa na kichwa kisemacho:"Njama za mauaji zafichuka"

Hata hivyo, Idara ya Usalama wa Taifa ilitoa taarifa za kukanusha kuhusika na utekaji wa Dk. Ulimboka na kuwataka wananchi wapuuze tuhuma hizo dhidi yao kwani ni za 'uzushi'.

Hii si mara ya kwanza kwa gazeti la Mwanahalisi kufungiwa. Mara ya mwisho, lilifungiwa kwa miezi mitatu kutokana na tuhuma zinazofanana na zile zinazotolewa sasa.

No comments:

Post a Comment