Wednesday, July 18, 2012

BOTI YAZAMA NA ABIRIA KIBAO ZANZIBAR, SPIKA AKATAA OMBI LA KUAHIRISHA BUNGE KWA DHARURA, KISHA AKUBALI BAADA YA KUOMBWA NA WAZIRI NCHIMBI.

Mhe. Spika, Anna Makinda

Mhe. Hamad Rashid Mohamed
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Anna Makinda, amekataa hoja ya Mbunge wa Wawi (CUF), Mh. Hamad Rashid Mohamed ya kutaka Bunge liahirishe shughuli zake leo jioni ili kutoa nafasi ya wabunge kwenda kuungana na wananchi wengine kushughulikia kuzama kwa boti ya abiria visiwani Zanzibar, ambayo inadaiwa kuwa na abiria zaidi ya 200.


Akizungumza bungeni muda mfupi uliopita, Spika Makinda alisema kuwa kanuni ya kutaka kuahirisha shughuli za Bunge kwa sababu ya dharura imekuwa ikitumiwa vibaya na hivyo akaikataa hoja ya Mhe. Hamad na badala yake akataka wabunge waendelee kujadili hoja iliyo mbele yao wakati serikali ikisaka taarifa kamili kuhusiana na ajali hiyo na kuchukua hatua zinazostahili.


Alisema kuwa kwa mujibu wa kanuni za Bunge, hoja ya dharura huwa na mashiko pale ambapo wabunge hulazimika kwenda kuungana na wananchi wengine kushughulikia tatizo lililotokea, akitoa mfano kuwa, ikiwa moto utatokea eneo jirani na bunge kama Chamwino, bunge linaweza kuahirishwa kwa dharura ili wabunge wakashirikiane na wananchi kushughulikia tatizo hilo kama vile kuzima moto huo, na pia hata kuchangia damu pindi ikilazimika kufanya hivyo.


Baada ya Spika kutoa ufafanuzi huo, wabunge wote wa Chama cha Wananchi (CUF) na vyama vingine vya upinzani walitoka nje ya ukumbi wa Bunge kutokana na kile kilichoonekana kuwa ni kumpinga Spika Anna Makinda kwa uamuzi wake wa kupinga hoja ya Mhe. Hamad.


WAZIRI NCHIMBI AONDOA HOJA, SPIKA ANYWEA
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Dk.Emmanuel Nchimbi.
Baada ya uamuzi wa Spika, uliombatana na kutoka nje kwa baadhi ya wabunge, Bunge liliendelea na shughuli zake ambapo Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani (ambayo ndiyo hushughulikia masuala ya uokoaji), alisimama na kutoa majibu ya baadhi ya hoja za wabunge.


Hata hivyo, baada ya naibu waziri kumaliza, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi alisimama na kusoma kanuni inayompa fursa ya kuomba kuondoa hoja yake na baada ya hapo, akamuomba Spika akubali kuahirisha kikao cha jioni hii (kama alivyoomba Hamad) ili wakapate nafasi ya kushughulikia ajali ya kuzama kwa boti hiyo.


Kufuatia ombi la waziri, safari hii Spika hakukataa. Alikubali kuwahoji wabunge waliobaki wa CCM juu ya hoja ya kuahirisha kikao cha jioni, na wote walikubali.
Boti hiyo iitwayo Skagit imezama leo wakati ikiwa katika eneo la Chumbe ikitokea jijini Dar es Salaam kuelekea Zanzibar baada ya kupigwa na wimbi kali na kupinduka.

No comments:

Post a Comment