Wednesday, July 18, 2012

BOTI SASA YAZAMA YOTE BAHARINI ZANZIBAR, WALIOOKOLEWA WAKIWA HAI WAFIKIA 145

Boti ya Skagit inavyoonekana kabla ya kuzama yote baharini.

Taarifa za hivi karibuni kutoka Zanzibar usiku huu zimedai kuwa hadi sasa, watu waliookolewa wakiwa hai ni 145 tu na pia maiti 14 zimeopolewa huku abiria wengine kadhaa kati ya wanaokadiriwa kufikia 250-300 waliokuwamo ndani ya boti ya Skagit iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kuelekea Zanzibar wakihofiwa kuzama.


Hivi sasa, boti hiyo iliyokumbwa na ajali katika eneo la Chumbe imezama kabisa na haionekani tena kama ilivyokuwa awali; huku juhudi zaidi za kuokoa abiria waliokuwamo zikiendelea kufanyika, ingawa ni kwa shida kwani hali ya bahari katika eneo la tukio si shwari.


Maelfu ya watu waliotaharuki visiwani Zanzibar wamekuwa wakikimbilia katika eneo la viwanja vya Maisara ambako turubai kubwa limefungwa.

Watu wamejazana Maisara kujaribu kutambua ndugu na jamaa waliokumbwa na ajali hiyo, huku vikosi vya uokoaji vikifikisha miili ya marehemu kila inapoopolewa baharini.

Kwa mujibu wa manusura wa ajali hiyo, ni kwamba boti waliyopanda ilianza kuzama baada ya kupigwa na wimbi kali na kupinduka.


Hadi sasa, hakuna taarifa zozote rasmi zilizotolewa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuhusiana na ajali hiyo. Tukio hilo  limetokea takriban mwaka mmoja tu tangu ajali nyingine ya kuzama kwa meli ya Mv Spice Islanders kwenye eneo la Nungwi kuua watu zaidi ya 2,000 wakati ikitokea Zanzibar kuelekea Pemba huku ikiwa imejaza watu kupita kiasi. 

No comments:

Post a Comment