Tuesday, July 24, 2012

BOCCO APIGA 'HAT-TRICK' SIMBA IKIAGA KAGAME

Wachezaji wa Azam wakimpongeza 'muuaji' wa Mnyama, John Bocco (katikati) wakati wa mechi yao ya robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo jioni. Azam ilishinda 3-1.
Mwinyi Kazimoto (kushoto) na  Felix Sunzu (kulia) wa Simba wakiwania mpira dhidi  Kipre Bolou wa Azam wakati wa mechi yao ya robo fainali ya Kombe la Kagame leo jioni.


Kipa wa Azam, Deogratius Munishi wa Azam (kushoto) akijiandaa kudaka mpira mbele ya straika wa Simba, Felix Sunzu wakati wa mechi yao ya robo fainali ya Kombe la Kagame kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo jioni. 
Winga Uhuru Selemani wa Simba (kulia) akipiga mpira mbele ya beki Ibrahim Shikanda (kushoto) huku Khamis Mcha (katikati) akijiandaa kutoa msaada wakati wa mechi yao ya robo fainali ya Kombe la Kagame kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo jioni.

Siku ya kufa nyani.... Kiungo mpya wa Simba, Mussa Mudde akitolewa kwa machela baada ya kuuamia vibaya mguu wake wakati wa mechi yao dhidi ya Azam kwenye Uwanja wa Taifa leo.

Mussa Mudde (katikati) akitoka uwanjani hukua kisaidiwa baada ya kuumia mguu katika mechi waliyolala kwa Azam leo.

Na Mwandishi Wetu
STRAIKA John Bocco 'Adebayor' alifunga magoli yote matatu na kuiwezesha timu yake ya Azam FC kutinga nusu fainali ya mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) kwa ushindi wa 3-1 dhidi ya Simba katika mechi yao ya robo fainali kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo jioni.

Kwa ushindi huo, Azam itacheza nusu fainali dhidi ya Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, ambayo mapema leo mchana iliwachapa Atletico ya Burundi 2-1 huku Taddy Etikiema wa Vita akifunga goli lake la 6 la mashindano hayo mwaka huu. Etikiema anafuatiwa na Said Bahanuzi wa Yanga mwenye magoli 5 katika mbio za kuwania kiatu cha mfungaji bora.

Nusu fainali ya pili kesho itakuwa ni baina ya Yanga na APR ambazo zitakutana kwa mara ya pili ndani ya wiki moja baada ya Ijumaa wenyeji kushinda 2-0 katika mechi yao ya mwisho ya Kundi C.

Azam walitawala sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza na juhudi zao zilizaa bao la kuongoza katika dakika ya 18 kupitia kwa Bocco aliyeunganisha kwa kichwa cha mkizi mpira wa krosi ya Ibrahim Shikanda na wangeweza kwenda mapumziko wakiongoza 2-0 kama wangepewa na kufunga penalti iliyoonekana kuwa ya wazi wakati mshambuliaji wao alipoangushwa ndani ya boksi.

Bocco, mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu ulioisha, aliifungia Azam bao la pili katika dakika ya 46 baada ya Uhuru Selemani kunyang'anywa mpira kirahisi na mfungaji kukimbia na mpira akitokea kulia mwa uwanja na kuingia ndani ya boksi kabla ya kupiga shuti lililomshinda kipa Juma Kaseja.

Simba walipata matumaini mapya ya kurejea mchezoni baada ya beki wa kushoto, Shomari Kapombe kufunga goli zuri la juhudi binafsi katika dakika ya 53, lakini shujaa wa Azam, Bocco, alimpeleka tena wavuni Kaseja kuokota mpira katika dakika ya 73 kwa shuti kali la nje ya 18 na kuandika bao lake la nne la michuano hii.   

Kipigo cha Simba kilihitimisha kampeni mbaya kwa mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo ambao wametwaa Kombe la Kagame mara 6, baada ya kufungwa mechi mbili (dhidi ya URA ya Uganda na Azam), sare moja (dhidi ya Vita Club) na kushinda moja tu (dhidi ya timu dhaifu ya Ports ya Djibout) kati ya nne walizocheza mwaka huu.

Baada ya mechi hiyo ambayo Azam walilipa kisasi cha kufungwa kwa penalti katika fainali ya Kombe la Urafiki wiki mbili zilizopita kwenye uwanja huo, kocha wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic alilalamikia muda mfupi wa maandalizi.

"Tulikuwa na siku 10 tu za kujiandaa. Michuano mikubwa kama hii unahitaji mwezi wa maandalizi," alisema Mserbia huyo ambaye timu yake ilikubali kwenda Zanzibar kushiriki kombe dogo la Urafiki ambalo halikuwepo kwenye ratiba huku mahasimu wao Yanga wakikataa na kupelekea timu ya vijana ambayo nayo ilikuja kutimuliwa na waandaaji chama cha soka cha Zanzibar (ZFA).

Kocha aliyejaa furaha wa Azam, Stewart Hall, aliwapongeza wachezaji wake kwa ushindi huo akisema walifuata maelekezo yake na kuweka juhudi kubwa uwanjani na akasisitiza kwamba walistahili ushindi mnono zaidi walikuwa na nafasi nyingi za kufunga na walinyimwa penalti.

"Nawapongeza wachezaji, wamecheza vizuri leo kuliko mechi iliyopita, wamefuata maelekezo yangu, wameweka juhudi. Tulikuwa na nafasi ya kupata ushindi mkubwa zaidi kwani tulitengeneza nafasi nyingi hasa kipindi cha kwanza na tulinyimwa penalti, ambayo kwangu ilikuwa ni penalti," alisema Hall.

Vikosi katika mechi ya jana jioni vilikuwa; Simba: Juma Nyosso, Mussa Mude/ Salim Kinje (dk. 83), Jonas Gerard Mkude/ Amri Kiemba (dk. 81), Mwinyi Kazimoto, Haruna Moshi 'Boban', Felix Sunzu na Uhuru Selemani/ Kigi Makasi (dk.66).

Azam: Deogratius Munishi 'Dida', Ibrahim Shikanda, Erasto Nyoni, Said Morad, Aggrey Morris, Kipre Bolou/ Ramadhani Chombo 'Redondo' (dk. 17), Kipre Tchetche/ George Odhiambo 'Blackberry', Salum Aboubakar, John Bocco 'Adebayor', Ibrahim Mwaipopo na Khamis Mcha/ Jabir Aziz (dk. 70).

No comments:

Post a Comment