Friday, July 20, 2012

FERGUSON: RIO FERDINAND HACHEZI TENA TAIFA ENGLAND


Rio Ferdinand
Ferguson akiingia na timu yake uwanjani wiki iliyopita katika mechi za maandalizi ya msimu nchini Afrika Kusini.
LONDON, England
KOCHA wa Manchester United, Sir Alex Ferguson amefichua kuwa hatarajii kumuona tena beki wake Rio Ferdinand akiichezea tena timu ya taifa ya England.
Licha ya kuwahi kuichezea timu ya taifa hilo mara 81, beki huyo wa kati aliachwa  katika kikosi cha awali cha nchi yake kilichoshiriki fainali za Euro 2012, na baadaye akatoswa tena licha ya beki aliyetrajiwa kutwaa mikoba yake, Gary Cahill kujiondoa kutokana na majeraha.

Kocha Roy Hodgson wa timu taifa ya England alisisitiza kwamba alichagua kikosi chake kwa kuzingatia sababu za kiufundi lakini Ferdinand alielezea kutofurahishwa kwake na hatua hiyo kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter, akigusia uvumi kwamba ameachwa kwa sababu ya mtafaruku uliopo baina ya John Terry na mdogo wake, Anton Ferdinand.

"Sidhani (kama Ferdinand ataichezea tena timu ya taifa ya England). Sioni uwezekano huo. Hilo halipo katika mipango yake," Ferguson aliwaambia waandishi wa habari.

"Sasa ana miaka 33  na anataka kuwa fiti ili aitumikie klabu yetu. Ukiwa kama beki wa kati, ukijitunza vizuri unaweza kucheza hadi kufikia miaka 37.

"Rio alicheza vizuri kwetu msimu uliopita. Pengine anaichezea kwa kiwango cha juu timu yetu na kwa muda mrefu kwa sababu alikuwa akicheza kila mara. Misimu miwili iliyopita amekuwa akicheza kila wiki, anakuwa nje kwa wiki tatu, halafu anarudi tena.

"Yeye na Jonny Evans walionyesha kiwango kizuri wakiwa pamoja na kuendelea hivyo kuanzia Desemba hadi Februari na Machi."
Wakati nahodha wa klabu hiyo, Nemanja Vidic akijiandaa kurejea kikosini baada ya kutumia muda mwingi wa msimu uliopita akiwa nje kutokana na jeraha la goti, Ferdinand anakabiliwa na ushindani mkali wa kuwanian namba katika kikosi cha kwanza, tofauti na msimu uliopita.

No comments:

Post a Comment