Wednesday, July 4, 2012

BAYERN WASHIKWA KIGUGUMIZI KUHUSU GUARDIOLA


Guardiola
BAYERN, Ujerumani
MKURUGENZI Mkuu wa Bayern Munich, Karl-Heinz Rummenigge alishindwa kutoa jibu la moja kwa moja wakati alipoulizwa juu ya taarifa kwamba wanataka kumchukua kocha Pep Guardiola, lakini akasema kwamba kocha Jupp Heynckes ataendelea kuinoa timu yao hadi mwishoni mwa mwaka 2012.

Hatma ya Heynckes katika kuiongoza Bayern iko shakani baada ya kumaliza katika nafasi ya pili kwenye michuano mitatu msimu uliopita, na kocha wa zamani wa Barca amekuwa akihusishwa na klabu hiyo.

Lakini, akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kumtambulisha Matthias Sammer kuwa mkurugenzi mpya wa michezo wa Bayern, Rummenigge alifichua kwamba klabu yao haitakurupuka kuhusiana na hatma ya kocha wao wa sasa.

"Tutafikiria kwa utulivu. Hamtapata maelezo yoyote kutoka kwetu kuhusiana na jambo hili kabla ya krismasi," Rummenigge aliwaambia waandishi wa habari.
"Baada ya hapo ndipo tutakapokaa na kuzungumza.
"Pep Guardiola? Hata mimi nimesoma habari hiyo, lakini hakuna yeyote kutoka Bayern ameithibitisha."

No comments:

Post a Comment