Tuesday, July 10, 2012

BALOTELLI AWATOA MACHOZI NDUGU ZAKE GHANA


*BABAKE MDOGO, SHANGAZI, BABU WAMUOMBA AENDE GHANA WALAU KUWASALIMIA TU

Baadhi ya ndugu wa Kibaiolojia wa Balotelli walioko Ghana

Namna hii Balotelli atarudi Ghana kweli? Afuate nini? Hapa ni katika pozi lake mojawapo la kula bata na vimwana akiwa majuu

Balotelli akiwa amevalia aina ya kofia ambayo aliwahi kumtumia baba yake mkubwa nchini Ghana na kuambatanisha na zawadi nyingine alizoanguka saini yake.
ACCRA, Ghana
Ndugu wa kifamilia nchini Ghana wa straika waManchester City, Mario Balotelli ameungana na maombi yaliyotolewa na wazazi wa kibaiolojia wa mchezaji huyo kumtaka arudi kwao mara moja.

Mario ni straika wa bei mbaya ambaye thamani yake ya sasa sokoni imepanda hadi kufikia paundi za England milioni 52 na ingawa alizaliwa Agosti 12, 1990 na wazazi Waghana, Rose na Thomas Barwuah, aliasiliwa na kulelewa na wazazi wake wa sasa wa Italia wakati akiwa na miaka mitatu kwa sababu ya matatizo ya kiafya aliyokuwa nayo. Alizaliwa mjini Palermo, kusini mwa Italia.
Hadi sasa kuna simulizi za aina mbili kuhusiana na namna Mario alivyochukuliwa na kulelewa na wazazi wake wa kurithi -- familia ya Muitalia Balotelli.

Mario alisema katika mahojiano yake kwamba alitelekezwa hospitalini na wazazi wake wa kibaiolojia, wa familia ya Barwuah.

Hata hivyo, Mzee Barwuah na mkewe wamekanusha madai hayo na kusisitiza kwamba, kilichotokea ni kuwa wao hawakuwa na fedha za kulipia ‘bili’ kubwa ya gharama za hospitali zilizotokana na matibabu yake, na kwamba, familia ya Balotelli ikatoa ofa ya kumtwaa kwa muda ili kumlea lakini kinyume chake hawakumrejesha na kumtwaa jumla.

“Kwanza hatukuwa na uhakika, lakini baadaye tukakubali kwa kuamini kwamba pengine uamuzi wao utakuwa na faida kwa Mario. Tulimuona kila wiki na kila kitu kilienda vizuri.

“Tulidhani kwamba kuna wakati, baada ya matatizo kwisha, Mario angerudi mikononi mwetu.
Lakini badala yake, kila mara tulipojaribu kumrudisha, familia ya Balotelli ikawa ikiongeza muda wa kutaka kuwa naye,” Mr. Barwuah aliliambia Daily Mail la Uingereza.

Tangu wakati huo, familia ya Barwuah imekuwa ikimsihi Mario kurejea mikononi mwao lakini kinyume chake akachukua uraia wa Italia wakati alipotimiza miaka 18 na mwishowe kubadilisha jumla jina la baba yake na kuwa Balotelli.

Mario amepuuza mwito wa ‘kurejea nyumbani’ na badala yake ameendelea kuwa gumzo duniani kwa mambo mawili anayotambua kwamba anayaweza sana: kucheza soka safi na kufanya mambo ‘kiukichaa’.

Hata hivyo, yapo matumaini kwa familia ya Barwuah kama Daily Record lilivyoandika kwamba ndugu wa ukoo wa Mario mjini kwao Konongo, Ghana, wameunga mkono kampeni ya kumsihi Mario arudi nyumbani ingawa wao hawajawahi kumtia mchoni.

Taarifa hizo zimemnukuu Alex Barwuah, 30, baba mdogo wa Mario, akisema: “Wote tunajivunia sana kwa ajili yake.

Tulifurahi sana wakati alipofunga mabao yote yaliyoipeleka Italia katika fainali ya michuano ya Euro 2012.Wakati alipovua jezi na kuonyesha kifua chake baada ya kufunga goli, marafiki zangu walinifanya na mimi nivue shati kama yeye.

Magoli yake yalinifanya nijihisi kuwa karibu naye. Sijawahi kukutana na Mario lakini najisikia furaha sana ninapomuona kwenye TV.

Huwa tunamtazama kadri inavyowezekana. Najisikia fahari kwamba yeye ni mmoja wa wanafamilia yetu.

“Hata hivyo najisikia vibaya kwa kutowahi kukutana naye, na kwamba baba yangu hajawahi kumuona mjukuu wake huyu … baba yangu alikuwa akitazama kila mechi inayomuonyesha Mario na pia kuwa na hamu sana ya kukutana naye, lakini haikuwezekana … naamini kwamba sasa Mario atakuja kuonana na sisi na kujifunza mambo ya mababu zake.”

Baba mkubwa wa Mario, Nana, dereva mstaafu wa mabasi, alifariki dunia hivi karibuni. Mario aliwahi mara moja kumpelekea zawadi ya kofia ya ‘baseball’ iliyokuwa na saini yake.
Taarifa pia zimesema kwamba Kwaku Awuah, babu yake Balotelli kwa upande wa mama, pia anamtaka mjukuu wake aende ‘nyumbani’ kwao kuwaona.

Kwaku, 80, alisema: “Inasikitisha kuwa na mjukuu nyota duniani lakini kutowahi kumtia machoni hata mara moja … najisikia vibaya sana kila mara ninapomuona kwenye TV au kumsoma magazetini …sihitaji fedha zake.
Ninachotaka ni kumwambia tu kwamba arudi kwenye mizizi yake kwa sababu, kuna msemo usemao, hakuna sehemu nzuri kama nyumbani kwako.”

Inaelezwa vilevile kuwa Akosua Osaa Barwuah, shangazi yake Mario na dada wa baba yake Thomas, pia anasikitishwa kuona kwamba hajawahi kukutana na mpwa wake.

“Najisikia vibaya kila mara ninapomuona kwenye TV…kaka yangu Thomas ameniletea picha ya Mario wakati alipokuwa na miaka mitatu.
Nina mpwa maarufu duniani ambaye sijawahi kukutana naye maishani mwangu,” alisema.


No comments:

Post a Comment