Tuesday, July 10, 2012

RAIS WA MADAKTARI AFUNGULIWA MASHTAKA MAHAKAMA YA KISUTU KWA KUHAMASISHA MGOMO WA MADAKTARI, AACHIWA KWA DHAMANA


Dk. Mkopi (kushoto) akisindikizwa kuingia mahakamani leo
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), leo amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka mawili yanayohusiana na mgomo wa madaktari na kusomewa mashtaka mawili kabla ya kuachiwa kwa dhamana.

Makosa aliyoshtakiwa nayo bosi huyo wa MAT ni ya kupuuza amri halali ya kusitisha mgomo na jingine ni la kuhamasisha mgomo huo.

Ilidaiwa mbele ya Hakimu Faisal Kahamba kuwa,  kati ya Juni 26 na Juni 28 mwaka huu, Mkopi alipuuza amri halali ya Mahakama Kuu (Divisheni ya Kazi), ya kuzuia mgomo wa madaktari na  badala yake kuhamasisha kuendelea kwa mgomo huo kinyume cha sheria. 

Rais huyo wa MAT alichiwa na Hakimu Kahamba baada ya kutimiza masharti ya dhamana, ambayo ni pamoja na kuwa na wadhamini wawili waliomdhamini kwa Sh. 500,000 kila mmoja.

Kesi hiyo ambayo imeahirishwa hadi Agosti 6, ilivuta hisia za watu wengi ambapo mamia ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam walifurika mahakamani hapo, wakiwemo madaktari walioonekana kumuunga mkono rais wao.No comments:

Post a Comment