Tuesday, July 10, 2012

REAL MADRID, BARCELONA KUVAANA AGOSTI 23 KATIKA 'EL CLASICO' YA KWANZA MSIMU HUU

Hoi! Lionel Messi wa Barca (kushoto) na Cristiano Ronaldo wakionekana kuchoka kama majogoo yaliyotoka kuzipiga katika mechi mojawapo ya 'el clasico' misimu miwili iliyopita.
MADRID, Hispania
REAL Madrid na Barcelona zitakutana katika mechi yao ya kwanza ya "Clasico" katika La Liga, Ligi Kuu ya Hispania mwishoni mwa wiki ya Oktoba 6-7 kwenye uwanja wa Barca wa Nou Camp, kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Soka Hispania (RFEF) mjini Madrid leo.

 Mabingwa Real baadaye watawakaribisha Barca, ambao walimaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa La Liga msimu uliopita, katika mechi watakayovaana mwishoni mwa wiki ya Machi 2-3, RFEF ilisema.

Mahasimu hao wa jadi watakutana mara mbili mwezi ujao katika mechi ya kuwania taji la Hispania la Super Cup, ambalo litawakutanisha mabingwa wa La Liga (Real) dhidi ya mabingwa wa Kombe la Mfalme (Barca).
 Mechi yao ya kwanza itachezwa Agosti 23 kwenye Uwanja wa Nou Camp, huku marudiano kwenye Uwanja wa Bernabeu yakiwa Agosti 30, kwa mujibu wa taarifa ya RFEF.
 Real wataanza kampeni zao za kuwania ubingwa wa La Liga kwa kucheza nyumbani dhidi ya Valencia,  walioshika nafasi ya tatu katika ligi hiyo msimu uliopita, ambapo watacheza mwishoni mwa wiki ya Agosti 18-19, wakati Barca wataanza kwa kuwakaribisha Real Sociedad.

 "Utakuwa msimu mgumu, kama ulivyokuwa msimu uliopita, na tutajaribu kufikia matarajio ya mashabiki wetu," Mkurugenzi wa Real, Emilio Butragueno alisema wakati wa upangaji ratiba.

 Real ya kocha Jose Mourinho iliweka rekodi kwa kufikisha pointi 100 wakati ikitwaa ubingwa kwa mara ya kwanza msimu uliopita baada ya kupita misimu minne, na kuhitimisha utawala wa Barca waliokuwa wametwaa ubingwa wa La Liga katika misimu mitatu mfululizo.


No comments:

Post a Comment