Wednesday, June 20, 2012

SAJUKI AREJEA, WASTARA AKERWA MADAI YA KUMDHALILISHA

Sajuki akiendeshwa katika kiti cha matairi kwenye Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam.

Na Amur Hassan

MUIGIZAJI maarufu nchini Juma Kilowoko a.k.a Sajuki amerejea nchini akitokea India alikoenda kwa matitabu akiwa na mkewe.


Mke wa muigizaji huyo, Wastara, amemwambia mtangazaji Zamaradi Mketema wa Radio Clouds FM katika kipindi cha LEO TENA kuwa Sajuki ana wiki sasa tangu aliporejea.


"Ana kama wiki sasa tangu arejee. Ni kweli kwamba nilikuwa nikiwaficha baadhi ya watu kuhusu kurejea kwa Sajuki kwa sababu sikufurahishwa na mambo niliyoyakuta huku.


"Watu wanaandika kwamba namdhalilisha Sajuki kwa kumpiga picha na kuzisambaza katika vyombo vya habari. Sajuki si kwamba hana akili. Ni mzima kiakili na kila kinachofanyika anakiona na anakuwa anatoa ridhaa. Siwezi mimi kumwambia lazima nikupige picha. Ikipigwa picha anakuwa ameridhia. 

"Na tunafanya hivyo kwa ajili ya kutoa ushirikiano kwa watu ambao wamejibana kutugharamia na kutuwezesha kwenda kupata matibabu hayo. Hao wanaoandika kwamba namdhalilisha ama siwapi ushirikiano wanajua tumeendaje India? Walitoa nini kutuchangia? Natoa ushirikiano kwa Clouds FM, Global Publishers, TBC kwa sababu wametoa mchango mkubwa katika kuifahamisha jamii kwamba tunahitaji msaada wa gharama za matatibu hadi Watanzania wakatuchangia. Sasa wewe unayesema namdhalilisha mume wangu una maana gani? Nimdhalilishe ili nipate nini?"


Wastara pia alielezea kukerwa na watu wanaovumisha kuwa Sajuki amefariki. "Si vizuri kuombeana mabaya. Unapowavumishia watu hivi unategemea nini. Watu wengine hawana uwezo wa kutafuta ukweli na huamini kila wanalosikia, unawapotosha. Kwani unaposema fulani kafa unadhani wewe utaenda wapi. Sajuki atakufa kwa mipango ya Mungu, mimi nitakufa na hata wewe unayesema hivyo hutadumu milele hapa duniani. Sajuki anaweza kukuzika wewe unayemvumishia uongo kwamba amekufa na kisha naye atakufa siku yake itakapofika kama mtu mwingine yoyote.


Wastara ambaye pia ni nyota wa filamu nchini, aliongeza: "Mtu anakuuliza Sajuki amepona? Sio kwamba amepona ila anaendelea vizuri kwa sababu bado kuna dawa anaendelea kutumia. Ila tunashukuru kwamba tumepata matibabu hata yale ambayo hatukutarajia na tunashukuru Mungu. Lililo la msingi ni kwamba tumuombee kwa Mungu ili hali yake isibadilike na aendelee vyema."

No comments:

Post a Comment