Wednesday, June 20, 2012

ENGLAND, UFARANSA ZATINGA ROBO-FAINALI EURO

WENYEJI UKRAINE WAJA JUU KUNYIMWA GOLI HALALI

Beki wa timu ya taifa ya England, Ashley Cole (kushoto) akimshuhudia mchezaji mwenzake John Terry (kulia) "akiosha" mpira wavuni wakati wa mechi yao ya Kundi D la Euro 2012 kwenye Uwanja wa Donbass Arena mjini Donetsk usiku wa kuamkia leo. Wenyeji walinyimwa goli hilo ambalo picha za marudio za televisheni zilithibitisha kuwa mpira ulitinga wavuni.
Mshambuliaji wa England, Wayne Rooney (wa pili kushoto) akisunga goli dhidi ya Ukraine wakati wa mechi yao ya Kundi D la michuano ya Euro 2012 kwenye Uwanja wa Donbass Arena mjini Donetsk usiku wa kuamkia leo.

WARSAW, Poland
ENGLAND iliwafunga wenyeji wenza Ukraine 1-0 na kutinga robo fainali ya Euro 2012 wakiwa vinara wa Kundi D usiku wa kuamkia leo, wakiivuka Ufaransa iliyomaliza katika nafasi ya pili baada ya kuchapwa 2-0 na Sweden.

Wayne Rooney alifunga kwa kichwa goli la mapema katika kipindi cha pili na kuwaweka England kileleni wakiwa na pointi saba na watawakabili washindi wa pili wa Kundi C, Italia, mjini Kiev Jumapili.

Ufaransa, ambao walimaliza na pointi nne, moja juu ya Ukraine, watawakabili mabingwa watetezi Hispania mjini Donetsk Jumamosi baada ya kupoteza nafasi yao ya uongozi kufuatia magoli mawili kutoka kwa Zlatan Ibrahimovic na Sebastian Larsson yaliyowapa Wasweden ambao walishatolewa mapema ushindi wa magoli "matamu".

Ibrahimovic alifunga goli la 'tik-taka'' akiwa ndani ya eneo la penalti baada ya kuiwahi krosi ya Larsson na kuwapa Wasweden uongozi katika dakika ya 54 kwa bao ambao bila ya shaka litaingia katika kinyang'anyiro cha kuwania tuzo ya goli bora la michuano. Larsson alifunga la pili katika dakika ya 90 kwa shuti kali la jirani ya lango lililotinga kwenye 'dari'.

Ulikuwa ni ushindi wa kwanza kwa Sweden dhidi ya Ufaransa tangu mwaka 1969 na kipigo cha kwanza cha Ufaransa katika 24 zilizopita.

Rooney, aliyekuwa amefungiwa mechi mbili za kwanza, alipoteza nafasi ya wazi ya kufunga katika kipindi cha kwanza lakini hakushindwa dakika mbili baada ya mapumziko wakati krosi ya Steven Gerrard ilipomshinda kipa Andriy Pyatov na kumwacha mshambuliaji huyo wa Manchester United akifunga katika nyavu tupu.

Ukraine, waliohitaji kushinda ili kusonga mbele, walinyimwa goli lao la kusawazisha katika dakika ya 62 wakati shuti la Marco Devic lilipozuiwa kidogo na kipa Joe Hart na kisha kuoshwa mstarini na John Terry.
Wachezaji wa Ukraine na mashabiki waliamini ni goli lakini refa wa nyuma ya lango aliwanyima haki yao na kuwaacha wenyeji wakijawa na hasira baada ya picha za marudio za televisheni kuonyesha kuwa mpira ulikuwa tayari umevuka mstari wa goli.

Mara mbili katika michuano mikubwa England, ambao walinyimwa goli kama hilo dhidi ya Ujerumani katika fainali za Kombe la Dunia 2010, wamejikuta katika matukio kama hayo yaliyoongeza presha ya kutaka kutumika kwa teknolojia ya mstari wa goli.

Kuongezwa kwa marefa wasaidizi wa nyuma ya lango, kuliletwa kwa kwa nia ya kuyaangalia kwa makini maamuzi ya katika mstari wa goli, lakini inaonyesha kwamba jana mwamuzi huyo hakumweleza refa kuwa ni goli, jambo lililomuacha kocha wa Ukraine, Oleg Blokhin, "akifura" kwa hasira.

Leo ni siku ya mapumziko ya michuano hiyo wakati mechi za robo fainali zitaanza kesho, ambapo Jamhuri ya Czech itaikabili Ureno mjini Warsaw.

No comments:

Post a Comment