Monday, June 18, 2012

RATIBA LIGI KUU ENGLAND YATOKA

Mabingwa Man City kuanza na wageni Southampton

Wachezaji wa Manchester City wakishangilia wakati walipotwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England msimu uliopita.

LONDON, England
MANCHESTER City wataanza kampeni za kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu ya England nyumbani dhidi ya timu iliyopanda daraja ya Southampton, kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana.

Washindi wa pili Manchester United wataanza kampeni zao ugenini dhidi ya Everton wakati msimu mpya wa ligi hiyo ya juu zaidi nchini England utakapoanza Agosti 18.

Reading waliorejea kwenye ligi kuu watawakaribisha Stoke, wakati timu nyingine iliyopanda daraja ya West Ham itawaalika Aston Villa.

Pambano la wataji wa jadi wa mji mmoja wa Manchester (The Manchester derby) litapigwa kwenye Uwanja wa Etihad Desemba 8 na marudiano kwenye Uwanja wa Old Trafford yamepangwa kuwa Aprili 6, 2013.

Kocha mpya wa Liverpool, Brendan Rodgers ataanza ajira yake kwa safari ya ugenini West Brom, ambayo sasa inafundishwa na kocha wa zamani wa Liver, Steve Clarke.

Liverpool, ambao kiwango chao duni msimu uliopita kilikuwa sababu ya kufukuzwa kwa kocha Kenny Dalglish, watazikabili Manchester City, Arsenal na Manchester United katika mechi zao tatu za kwanza za nyumbani.

Michael Laudrup, ambaye amechukua nafasi ya Rodgers klabuni Swansea, atakuwa ugenini dhidi ya QPR.
Utawala wa Paul Lambert kama kocha wa Aston Villa utaanza kwa safari ya ugenini dhidi ya washindi wa mechi ya "kapu" ya kuamua timu ya kupanda kwenye ligi kuu, West Ham, kabla ya kurejea kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Villa Park dhidi ya Everton.

Kocha mpya wa Norwich, Chris Hughton atakuwa na mtihani mgumu katika mechi yake ya kwanza wakati watakapoenda ugenini Fulham.

Arsenal wataanza kwa kuwakaribisha Sunderland na kocha Roberto Di Matteo atafanya kazi yake kwa mara ya kwanza kama kocha wa kudumu wa mabingwa wa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya Chelsea ugenini dhidi ya Wigan.

Tottenham wamepewa mwanzo mgumu kwa safari ya ugenini Newcastle.

Mechi ya kwanza ya wapinzani wa jadi wa Merseyside baina ya Everton na Liverpool itachezwa kwenye Uwanja wa Goodison Park Oktoba 27.

Chelsea watasafiri kwenda kuwakabili Arsenal Septemba 29 na mechi ya wapinzani wa London kaskazini baina ya Gunners na Tottenham imepangwa kuwa Novemba 17 kwenye Uwanja wa Emirates.

Sunderland na Newcastle watavaana Oktoba 20 kwenye Uwanja wa Stadium of Light wakati Newcastle watawakabili Manchester United kwenye Uwanja wa Old Trafford wakati wa "Boxing Day".

Manchester City watawakabili Norwich nyumbani katika siku ya mwisho wa msimu, huku majirani zao Man United watasafiri kwenda West Brom. Chelsea watamaliza msimu na Everton kwenye Uwanja wa Stamford Bridge wakati Arsenal watamaliza msimu wao ugenini dhidi ya Newcastle.

No comments:

Post a Comment