Monday, June 18, 2012

KOCHA UHOLANZI ACHUNIA KUJIUZULU

Wachezaji wa timu ya taifa ya Uholanzi wakijiuliza baada ya kufungwa goli la pili dhidi ya Ureno usiku wa kuamkia leo.


KOCHA wa timu ya taifa ya Uholanzi, Bert van Marwijk amekataa kujibu maswali kuhusu hatma yake baada ya taifa lake kutolewa kwa aibu katika hatua ya makundi ya fainali za Euro 2012.

Baada ya kutajwa kama moja ya timu zinazopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa michuano hiyo ya mataifa ya Ulaya, Waholanzi walitolewa kufuatia kipigo cha 2-1 kutoka kwa Ureno, ambacho kilikuwa kipigo chao cha tatu katika mechi tatu za Kundi B lililokuwa likitajwa kama "kundi la kifo".

"Mnaweza kuniuliza maswali ya aina zote, lakini si kuhusu hatma yangu," kocha huyo wa zamani wa Feyenoord alisema.

Hata hivyo, kocha huyo mwenye umri wa miaka 60 alisema anakubali kubeba yeye mzigo wa lawama zote kufuatia kutolewa na Ureno.

Uholanzi ambayo ilifungwa katika mechi ya fainali ya Kombe la Dunia 2010 ilijua kwamba inahitaji ushindi dhidi ya kikosi cha kocha Paulo Bento ili kuangalia uwezekano wa kutinga robo fainali.

Kipigo kisichotarajiwa cha 1-0 katika mechi ya ufunguzi dhidi ya Denmark, kilifuatiwa na kipigo cha 2-1 kutoka kwa wapinzani wao wa jadi Ujerumani katika mechi ya pili ha makundi, viliiacha Uholanzi ya Van Marwijk ikiwa na mlima mkubwa wa kupanda ili kusonga mbele.

Alijibu kwa kuwapanga washambuliaji wawili Rafael van der Vaart na Klaas-Jan Huntelaar pamoja na Robin van Persie katika kikosi cha kwanza katika mechi hiyo ya juzi iliyochezwa mjini Kharkiv.

Goli kali la shuti la "mkunjo wa ndizi" kutoka kwa Van der Vaart liliwapa Wadachi matarajio kiasi kabla ya nahodha wa Ureno, Cristiano Ronaldo kuwafunga magoli mawili "matamu" yaliyosambaratisha.

"Tulijua kwamba tulihitaji kushinda kwa togfauti ya magoli mawili hivyo tutaamua kucheza kamari kwa kupanda mbele kushambulia," alisema Van Marwijk.

"Wakati mwingine inafanya kazi na wakati mwingine inagoma. Nadhani tulianza mechi vizuri sana leo na kufunga ndani ya dakika 10.

"Lakini mliona tulipofungwa goli, matumaini yalibaki. Kama tungefunga la pili, tungejiamini zaidi, lakini hatukutumia nafasi zetu.

"Tumefadhaishwa. haikuwa mechi nzuri hata kidogo leo. Nawajibika kwa yaliyotokea na nimefadhaika."

No comments:

Post a Comment