Saturday, June 16, 2012

Poulsen, Samatta watamba ushindi upo Msumbiji

Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen (katikati) na nahodha wa timu hiyo Juma Kaseja (kulia) na mshambuliaji Mbwana Samatta wakizungumza mjini Maputo jana kuhusu mechi yao na Msumbiji leo (Jumapili) katika Uwanja wa Zimpeto.

Na Mwandishi Maalumu, Maputo
KOCHA wa timu ya taifa ya soka ya Kilimanjaro Taifa Stars, Kim Poulsen amesema kikosi chake kina kazi kubwa katika mechi ya kesho dhidi ya wenyeji Msumbuji, lakini ushindi ni lazima.

Katika mechi ya kwanza iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Stars ilitoka sare ya bao 1-1 na Msumbiji ‘Mambas’. Mechi ya kesho itachezwa kwenye Uwanja wa Taifa wa Zimpeto jijini hapa.
Akizungumza jana mjini hapa, Poulsen alisema wachezaji wake katika morali ya hali ya juu na wanachotaka ni kushinda mchezo wa kesho.

“Msumbiji ni timu nzuri, wanacheza kwa kasi na kila kitu nimekifanyia kazi. Ninaamini tutafanya vizuri, kikubwa ni kufuata maelekezo ya kila tunachotakiwa kufanya,” alisema kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya vijana ya U-20 anayeiongoza Stars katika mechi yake ya nne tangu aliporithi mikoba ya Mdenmark mwenzake Jan Poulsen ambaye hakuongezwa mkataba.

Katika mechi zake tatu za kwanza, Kim alishinda mechi moja (2-1) dhidi ya Gambia, alifungwa moja (2-0) dhidi ya Ivory Coast na kutoka sare moja (0-0) dhidi ya Malawi.

Stars ambayo inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania kupitia bia ya Kilimanjaro Premium Lager, ilitua hapa Ijumaa na kufanya mazoezi juzi na jana ilitarajia kufanya mazoezi ya mwisho kabla ya mechi hiyo ya kuwania kucheza fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika nchini Afrika Kusini Januari mwakani.

Nahodha wa Stars, Juma Kaseja alisema ana imani kubwa na kikosi chake ambacho kitacheza kwa kujituma.

"Tunataka ushindi na tumejiandaa vilivyo, tunajua Msumbiji ni timu nzuri lakini inafungika. Morali yetu iko juu na kitu muhimu ni ushindi," alisema.

Naye mshambuliaji Mbwana Samatta anayecheza soka la kulipwa katika klabu ya TP Mazembe ya DRC, alisema wanaiheshimu Msumbiji lakini bado wanachotaka hiyo kesho ni ushindi.

"Tunawaheshimu, lakini hii haina maana kwamba tunawahofia, tunataka ushindi. Tutajitahidi kadri ya uwezo wetu kufanya vizuri," alisema.

No comments:

Post a Comment