Saturday, June 16, 2012

NANI AMTETEA RONALDO KUKOSA MAGOLI

Shuti la Cristiano Ronaldo wa Ureno (kushoto) likiokolewa na kipa Stephan Andersen wa Denmark wakati wa mechi yao ya Kundi B la UEFA Euro 2012 kwenye Uwanja wa Arena Lviv mjini L'viv, Ukraine Juni 13, 2012.

WINGA wa Manchester United, Nani amemtetea mchezaji mwenzake wa timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo kwa shutuma anazopata kutokana na kiwango chake katika fainali za Euros 2012.

Nani amemtetea Ronaldo akisema nyota huyo wa Real Madrid "hana sababu ya kuhofia chochote" licha ya yaliyotokea katika katika mechi dhidi ya Denmark Jumatano.

"Yuko sawa, ana furaha kwa sababu tulishinda mechi ile. Hakuna cha kuhofia," Nani alisema kuhusu nyota mwenzake huyo wa zamani wa Manchester United. "Katika mechi, kila mtu anapoteza nafasi. Alikuwa na nafasi nzuri ya kufunga, hakufunga, lakini bado tunayo mechi inayofuata. Pengine katika mechi hiyo inayokuja yeye ndiye atakayeamua matokeo yetu.

"Tunahitaji kila mmoja awe katika kiwango chake bora kwa sababu Cristiano hachezi peke yake na tuna wachezaji wakali katika kikosi hiki. Hakika, yeye ni mchezaji muhimu sana kwetu. (Lakini) yuko poa kabisa. Amefanya mazoezi vyema, mchango wake kwa timu ni mkubwa … yuko vizuri. Anasaidia ulinzi, anashambulia, hakufunga goli katika nafasi aliyopata lakini nina hakika kwa asilimia 100 kwamba ataisaidia timu na kwamba kila mmoja anayecheza atafanya hivyo."

No comments:

Post a Comment