Thursday, June 28, 2012

OKWI KUBEBA TUZO YA MCHEZAJI BORA LIGI YA VODACOM J'MOSI?

Emmanuel Okwi (kulia) na makamu mwenyekiti wa Simba, Godfrey Nyange 'Kaburu' wakionyesha alama ya vidole vitano baada ya kuwadhalilisha mahasimu wao Yanga kwa kipigo cha 5-0 katika mechi ya kufungia msimu uliopita ambapo Okwi alifunga magoli mawili na kupika mengine mawili.
KAMPUNI ya huduma za simu ya Vodacom itakabidhi zawadi kwa washindi wa Ligi Kuu ya Vodacom msimu 2011/2012 katika hafla itakayofanyika kesho Jumamosi Juni 30, 2012 kwenye hoteli ya Double Tree Hilton jijini Dar es Salaam.

Hafla hiyo itakayohudhuriwa na wawakilishi wawili kutoka katika kila klabu ya Ligi Kuu itaanza saa 12 jioni. Katika hafla hiyo washindi mbalimbali wakiwemo bingwa, makamu bingwa na mshindi wa tatu.

Simba ndio mabingwa wa msimu uliopita wakifuatiwa na Azam, pamoja huku Yanga wakishika nafasi ya tatu.

Wengine watakaozawadiwa ni mfungaji bora, kipa bora, timu bora yenye nidhamu, mchezaji bora wa ligi, refa bora na kocha bora.

Mshambuliaji wa Azam, John Bocco, alimaliza ligi akiwa mfungaji bora, huku tuzo ya mchezaji bora wa ligi ikitarajiwa kwenda kwa kiungo wa Simba, Mganda Emmanuel Okwi, ambaye pia alimaliza wa pili katika orodha ya wafungaji bora na huku akiisaidia timu yake kutwaa ubingwa wa ligi hiyo.

Kipa Juma Kaseja anapewa nafasi kubwa kutwaa tuzo ya kipa bora kutokana na kuruhusu magoli machache na kuipa ubingwa Simba kutoka kwa mahasimu wao Yanga.

Aidha, tuzo ya kocha bora huenda ikatua kwa Mserbia Milovan Cirkovic kwa kuipa Simba ubingwa.

No comments:

Post a Comment