Na Moshi Lusonzo

TAMASHA la Fiesta - 2012 litakuwa la aina yake baada ya waandaaji kutenga Sh. milioni 250 kwa ajili ya zawadi mbalimbali ikiwemo magari watakayopewa mashabiki.

Akizungumza na waandishi wa habari, mratibu wa tamasha hilo Sebastian Maganga alisema pamoja na zawadi hiyo, Fiesta ya mwaka huu itakayoanza Julai itahusisha nchi mbili za Tanzania na Kenya.

Alisema kwa Tanzania wamepanga kutembelea mikoa 14 tofauti na mwaka jana na Kenya watafanya kwenye jiji la Nairobi ili kuwapagawisha mashabiki wa muziki.

Maganga alisema ili kuweka wigo mpana wameamua katika matamasha hayo kuchukua wanamuziki wachanga pamoja na wakonge ili kuongeza ladha na kuibua vipaji.

"Mwaka huu tumeamua kuongeza ladha ya Fiesta, tunawaibua wale wenye ndoto ya muziki na pia kuwaonyesha wakongwe wa muziki waliobakia ili kuonyesha utajiri wetu na kukidhi kiu ya wananchi," alisema Maganga.

Akizungumzia zawadi hiyo, Maganga alisema mashabiki watapata fursa ya kujishindia magari sita aina ya Vitz, pikipiki 14, Sh. milioni 1 kwa wiki katika michezo ya kubahatisha. Pia zawadi nyingine ni Sh. 100,000 kila siku pamoja na simu za mikononi.