Thursday, June 28, 2012

DEL BOSQUE: HISPANIA TUMEWAFUNGA URENO KIBAHATI



Del Bosque


DONETSK, Ukraine
HISPANIA walisaidiwa na bahati kutinga fainali ya tatu mfululizo ya michuano mikubwa na Ureno ndio waliocheza vizuri katika muda mwingi wa mechi, alisema kocha Vicente del Bosque wa Hispania baada ya kushinda kwa penati 4-2 katika nusu fainali yao ya Euro 2012.

Mahasimu hao hawakufungana katika dakika 90 za kawaida na pia katika muda wa ziada uliowafanya wamalize mechi hiyo kwa dakika 120, lakini walionyesha soka safi na lenye ushindani mkali katika muda wote.

Matokeo ya penati yalitegemea ni timu gani yenye bahati zaidi ambapo mwishowe mabingwa wa Dunia na Ulaya waliibuka kidedea.
Wakati Hispania wakiongoza kwa penati 3-2, Bruno Alves wa Ureno alishuhudia penati yake ikirudi uwanjani baada ya kugonga ‘besela’ huku ya Cesc Fabregas iliyogonga pia mlingoti wa goli ikijaa wavuni na kuwapa ushindi Hispania.

"Tulikuwa na bahati sana wakati wa upigaji wa penati," Del Bosque aliuambia mkutano na waandishi wa habari.
"Lakini napenda kutoa pongezi zangu kwa timu ya Ureno kwa sababu walionyesha soka zuri, lakini sisi tulikuwa na bahati, kwakweli safari hii tulikuwa na bahati sana."

Alisema vilevile kuwa kwa ujumla, Ureno walicheza vizuri zaidi, wakijilinda vizuri mara kadhaa kuliko Hispania na kuonekana hatari wakati wakishambulia, lakini wachezaji aliowaingiza,  Jesus Navas na Pedro badala ya David Silva na Xavi, walibadili kila kitu.
"Tulitengeneza nafasi nyingi za kufunga wakati walipoingia, tuliwashambulia zaidi na ilikuwa muhimu kuwaingiza. Tulionekana kuchoka na hivyo tulihitaji kasi ya ziada, hasa katika dakika za nyongeza wakati Pedro alipoingia," alisema.

Del Bosque alisema kuwa hakupata ugumu wowote kuchagua wachezaji wa kupiga penati kwani Xabi Alonso (aliyekosa), Andres Iniesta, Gerard Pique, Sergio Ramos na Fabregas wote ni wapigaji makini.

"Hakukuwa na tatizo, Cesc aliniambia kwamba anataka kupiga penati ya mwisho itakayotupa ushindi na ndivyo alivyofanya,"  aliongeza.

Kwa ushindi huo, Hispania watacheza fainali ya Euro 2012 itakayofanyika Jumapili dhidi ya mshindi wa nusu fainali nyingine kati ya Italia na Ujerumani.

No comments:

Post a Comment