MICHUANO YA KAGAME KUANZA JULAI 14
MASHINDANO ya Klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la
Kagame) yanayoandaliwa na Baraza la Vyama ya Mpira wa Miguu Afrika
Mashariki na Kati (CECAFA) yatafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia
Julai 14-29 mwaka huu ambapo timu zinatakiwa kuthibitisha ushiriki wao
kabla ya Juni 25 mwaka huu.
Yanga itashiriki mashindano hayo ikiwa bingwa mtetezi, wakati
Tanzania Bara itawakilishwa na mabingwa wake Simba na washindi wa pili
Azam. Mashindano hayo yatafanyika jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja wa
Taifa na Uwanja wa Chamazi pekee kwa sababu ya kupunguza gharama za
uendeshaji.
Ratiba ya mashindano hayo yanayoshirikisha mabingwa kutoka nchi
kumi na moja ambao ni wanachama wa CECAFA itapangwa Juni 29 mwaka huu.
Mashindano haya ni muhimu kwa CECAFA na Tanzania Bara ambayo ndiyo
mwenyeji kwa maendeleo ya mpira wa miguu na pia kukuza kiwango cha
mchezo huo kwa ukanda huu ambao kwa Afrika unaoongoza kwa kufanya
mashindano mengi ya timu za Taifa pamoja na klabu.
Mwenyekiti wa CECAFA ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amewaomba wadau kujitokeza
kudhamini michuano hiyo ambayo itaoneshwa na kituo cha televisheni cha
SuperSport. Pia amewataka mashabiki kujitokeza kwa wingi viwanjani
kuunga mkono michuano hiyo.
CECAFA inawashukuru wadau wote kwa kuwezesha michuano hiyo
kufanikiwa akiwemo Rais wa Rwanda, Paul Kagame kwa kutoa zawadi za fedha
kwa washindi, Serikali ya Tanzania kwa kutoa Uwanja wa Taifa na Kamati
ya Utendaji ya TFF kwa kukubali kuwa mwenyeji wa mashindano hayo.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Mjumbe, Kamati ya Habari CECAFA
No comments:
Post a Comment