Friday, June 22, 2012

NAHODHA MPYA SENEGAL PAPISS CISSE ALONGA

Nahodha mpya wa timu ya taifa ya Senegal, Papiss Cisse (kulia) akiwa na Demba Ba (kushoto) wakati wa moja ya mechi za timu hiyo ya taifa.

NAHODHA mpya wa timu ya taifa ya Senegal, Papis Cisse amesema mafanikio kwenye timu yanatokana na ushirikiano wa wachezaji wote si nahodha pekee.
"Mafanikio ni zaidi ya nahodha," alisema Cisse. "Ni kazi inayohitaji ushirikiano wa timu."

Mdunguaji huyo alishindwa kung'aa katika fainali za Mataifa ya Afrika 2012 nchini Gabon na Equatorial Guinea ambapo alishuhudia timu yao ya taifa iliyokuwa ikipewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa michuano hiyo ikitolewa katika hatua ya makundi kufuatia kufungwa mechi zote tatu. 

"Yaliyopita yamepita. Tujipange huku tukitarajia kwamba tutafuzu kucheza AFCON 2013 na Kombe la Dunia 2014," alisema.

"Kwa kikosi cha vijana tulichonacho tunaamini tutaongezeka ubora," alisema.

Watoto wa shule ya soka ya Newcastle wakifurahi na kushangaa baada ya Papiss Cisse kufanya ziara ya kuwastukiza ambayo hawakutaarifiwa.
Cisse ametengeneza jina katika kipindi kifupi tangu alipotua kwenye Ligi kuu ya England akiwa na klabu yake ya Newcastle, huku akishikilia rekodi ya mchezaji Mwafrika wa kwanza nchini Ujerumani kufunga magoli mengi ya ligi katika msimu mmoja baada ya kupachika mabao 22 katika msimu wa Bundesliga 2010–11. Katika msimu huo pia alipewa tuzo ya EFFIFU kwa kuwa mshambuliaji makini zaidi wa Bundesliga.

Magoli hayo 22 pia yalimfanya kuweka rekodi kwa klabu yake ya zamani ya Freiburg ya mchezaji wa klabu hiyo aliyepata kufunga magoli mengi zaidi kwenye ligi katika msimu mmoja. Rekodi ya awali kwa Mwafrika kufunga magoli mengi Bundesliga ilikuwa ikishikiliwa na Tony Yeboah ambaye alifunga magoli 20 akiwa na klabu ya Eintracht Frankfurt mwaka 1993.

Katika msimu huo pia alikuwa mfungaji bora wa pili katika Bundesliga, nyuma ya Mario Gomez wa Bayern Munich aliyefunga magoli 28.

Cisse alijiunga na klabu ya Bundesliga ya SC Freiburg Desemba 28, 2009 akitokea FC Metz ya Ufaransa kwa ada ya uhamisho ya euro milioni 1.6.

Januari 17, 2012, Cisse akajiunga na Newcastle United kwa mkataba wa miaka mitano na nusu kwa ada inayokadiriwa kuwa paundi milioni 10 kulingana na mechi atakazocheza na magoli atakayofunga katika safu ya ushambuliaji anayoshirikiana na Msenegal mwenzake, Demba Ba.

Tangu alipotua Newcastle Januari mwaka, Cisse alicheza mechi 14 na kufunga magoli 13 ya ligi msimu uliomalizika.

Goli lake la 12 na la 13 aliyafunga katika ushindi wa 2–0 dhidi ya Chelsea kwenye Uwanja wa Stamford Bridge Mei 2, 2012, huku goli lake la pili ambalo mwenyewe amelielezea kuwa ndilo bao bora la maisha yake ya soka, likishinda tuzo ya BBC ya Goli Bora la Msimu.

No comments:

Post a Comment