Friday, June 22, 2012


KELVIN YONDANI AKATA MZIZI WA FITINA

Kelvin Yondani akiwa katika jezi mpya ya Yanga akijifua kwenye uwanja wa mazoezi wa klabu hiyo wa Kaunda leo asubuhi.


HATIMAYE aliyekuwa beki wa kutumainiwa wa klabu ya Simba katika msimu uliopita Kevin Yondan "Vidic" leo amekata mzizi wa fitina baada ya kuanza rasmi mazoezi  katika uwanja wa Kaunda uliopo Makao Makuu ya klabu ya Yanga na kuwa kivutio katika mazoezi hayo.

Kipenzi hicho cha Yanga kiliwasili majira ya saa tatu kasoro dakika kumi asubuhi, ambapo mara baada ya kushuka katika gari, mashabiki waliofurika katika mazoezi hayo walipomuona ghafla walimshangilia kwa vifijo na nderemo huku akielekea uwanjani akiwapungia mikono mashabiki hao.

Vidic ambaye ana mapenzi makubwa na klabu ya Yanga, leo ameripotiwa na chombo  kimoja cha  habari kuwa eti alitekwa hapo jana  na klabu ya Simba na kudaiwa kushiriki katika mazoezi na timu yake hiyo ya zamani.

Mchezaji huyo ambaye kila kukicha timu yake hiyo ya zamani imekuwa ikiendelea kumuota kwa mazuri aliyowafanyia, amekuwa gumzo kwa kipindi hiki cha usajili ambapo timu yake mpya ya Yanga imeendelea kufanya kufuru ya usajili ambao unatarajiwa kumalizika Julai 15 mwaka huu.

Yondani hivi karibuni aliwashukuru wanachama na wapenzi wa klabu ya Simba kwa ushirikiano aliokuwa akiupata wakati akiitumikia timu hiyo, aliweka bayana mara baada ya kumwaga wino kuichezea Klabu ya Yanga kuwa Simba isihangaike na yeye kwakuwa hana mpango tena wa kuichezea klabu yake ya zamani.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida mwanachama mmoja wa klabu ya Simba muda mfupi uliopita wakati www.youngaficans.co.tz ikiwa mitamboni aliwasili katika mazoezi ya timu ya Yanga yaliyokuwa yakifanyika katika uwanja wa Kaunda kwa ajili ya kutaka kuhakikisha juu ya uvumi wa beki Kevin Yondan kuwa yupo katika mazoezi.

Mara baada ya kumshuhudia mchezaji huyo akifanya mazoezi mwanachama huyo aliangua kilio uwanjani hapo huku mashabiki wa Yanga wakishangilia na kumnunulia maji ya matunda pamoja na uji.

Wachezaji wengine walioanza mazoezi leo ni pamoja na kiungo wa timu ya taifa, Frank Domayo aliyetokea klabu ya JKT Ruvu na mshambuliaji yosso wa timu ya taifa, Saimon Msuva aliyekuwa Moro United.

Naye Kocha msaidizi wa Klabu ya Yanga, Fredy Felix Minziro amesema kikosi chake chote  kinatarajiwa kukamilika mara baada ya wachezaji Haruna Niyonzima aliyekuwa na timu ya taifa lake (Rwanda) na Rashid Gumbo anayeumwa malaria watakapojiuunga na kikosi hicho.

Wachezaji waliofanya mazoezi leo ni:

Walinda mlango: Yaw Berko, Said Mohamed na Ally Mustapha 'Barthez'

Walinzi wa pembeni: Shadrack Nsajigwa, Godfrey Taita, Oscar Joshua na Juma Abdul,

Walinzi wa kati: Kelvin Yondani, Nadir Haroub 'Cannavaro', Ibrahim Job, Ladislaus Mbongo,

Viungo wa Ulinzi: Juma Seif Kijiko, Athuman Idd 'Chuji' , Salum Telela 'Essien',

Viungo wa Pembeni: Shamte Ally, Idrisa Rashid 'Messi', Omega Seme

Viungo washambuliaji: Nizar Khalfan, Frank Domayo, Nurdin Bakari 'Tshabalala'

Washabuliaji: Hamis Kiiza 'Diego', Jeryson Tegete, Said Bahanunzi, Simon Msuva

CHANZO: www.youngafricans.co.tz

No comments:

Post a Comment