Saturday, June 16, 2012


MCHAKATO KUMRITHI NCHUNGA YANGA WANOGA
Makao Makuu ya klabu ya Yanga jijini Dar es Salaam


KAMATI ya Uchaguzi ya TFF jana ilisema katika taarifa yake kwa wadau na wapenzi wa soka kuwa mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa YANGA kujaza nafasi zilizowazi za Kamati ya Utendaji unaendelea vizuri chini ya Kamati ya Uchaguzi ya YANGA.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na Idara ya Habari ya TFF, kamati ya uchaguzi ya shirikisho hilo la soka nchini imepokea kutoka kwa Kamati ya Uchaguzi ya YANGA nakala za fomu za maombi ya uongozi wa YANGA pamoja na nakala za vyeti vya elimu vya waombaji uongozi kama sehemu ya taarifa ya awali ya mchakato wa uchaguzi huo wa YANGA.
"Kamati ya Uchaguzi ya TFF imebaini kuwa baadhi ya waombaji uongozi wamewasilisha nakala za vyeti vya kuhudhuria masomo ya sekondari (Secondary School Leaving Certificate) badala ya nakala za vyeti vya kuhitimu masomo ya elimu ya sekondari (Certificate of Secondary Education)," ilisema taarifa hiyo.
Iliongeza: "Kamati ya Uchaguzi ya TFF imekwisha ielekeza Kamati ya Uchaguzi ya YANGA kuwataka wagombea wote kuzingatia Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara ya 10(4) na (5) inayowataka wagombea wote kujaza Fomu Na.1 ya maombi ya uongozi na kuambatanisha nakala ya cheti cha Elimu ya Sekondari (Certificate of Secondary Education) kama ilivyoainishwa kwenye Fomu Na.1 kipengele Na.9. Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeiagiza Kamati ya Uchaguzi ya YANGA iwashauri wagombea ambao vyeti vyao vimepotea wawasiliane na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) kwa maandishi ili kupata ‘Statement of Examination Results’ itakayotumwa kwa Kamati ya Uchaguzi ya YANGA kupitia TFF kuthibitisha kuwa wamehitimu elimu ya kidato cha nne."
Uhakiki wa vyeti vya elimu ya sekondari vya waombaji uongozi hufanywa na NECTA na vyuo husika kwa elimu ya juu kwa chaguzi za wanachama wa TFF hivyo kutokana na hilo wanachama wote wa TFF wameambiwa kuwa wanatakiwa kuzingatia kikamilifu matakwa ya Kanuni za Uchaguzi.
Nafasi zinazotarajiwa kujazwa ni pamoja na ya mwenyekiti kufuatia kujiuzulu kwa Lloyd Nchunga na nyingine za Makamu Mwenyekiti na za wajumbe.

No comments:

Post a Comment