Monday, June 18, 2012

KIM: KATIKA PENALTI YEYOTE ANAWEZA KUSHINDA

Mbwana Samata (kushoto) wa Taifa Stars akipiga mpira mbele ya mchezaji wa Msumbiji wakati wa mechi yao ya kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwenye Uwanja wa Taifa ulioko Zimpeto pembeni kidogo ya Jiji la Maputo. Stars ililala kwa penalti 7-6 baada ya sare ya 1-1.

MAPUTO, Msumbiji
KOCHA wa Tanzania, Kim Poulsen amesema baada ya kupoteza mechi dhidi ya Msumbiji sasa atajipanga upya kwa ajili ya mashindano yajayo kwani timu yake imeonyesha uwezo mkubwa katika mechi hiyo ya Jumapili.

Kim alishuhudia Taifa Stars, ambayo kwa sasa inadhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, ikiondolewa na Msumbiji kwa penalti 7-6 baada ya kumaliza dakika 90 kwa sare 1-1 kwenye mchezo huo wa kusaka kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika 2013.

Akizungumza na vyombo vya habari, Kim alisema Stars walicheza vizuri lakini The Mambas walitumia nafasi nzuri ya kuwa nyumbani na kushinda.

"Nawapongeza kwa kushinda, lakini najivunia vijana wangu kwa jinsi walivyocheza kwa umakini muda wote wa mchezo huu.

"Nilijua Msumbiji wangeshambulia kwa nguvu, lakini na sisi tulicheza soka letu la kawaida na kutegeneza nafasi nyingi. Nashukuru tulisawazisha lakini inapofikika hatua ya kupigiana penalti lolote linaweza kutokea."

Naye kocha wa Msumbiji, Gert Engels aliwasifu Stars kwa kucheza vizuri, huku akiwapongeza wachezaji wake kwa kushinda mchezo huo.

"Tanzania ni timu nzuri inacheza kwa uelewano mkubwa, lakini wakati wa mapumziko niliwaambia wachezaji wangu watulie na wacheze kama nilivyoowaagiza," alisema Engels.

"Tanzania wanapaswa kuitunza hii timu kwa sababu ina wachezaji wengi chipukizi wenye vipaji vya hali ya juu, ni bahati mbaya tu tumewafunga kwenye penalti."

Naye beki Erasto Nyoni alisema wamepokea kwa masikitiko matokeo hayo lakini akaahidi kuisaidia timu hiyo kwenye michezo mingine.

"Tunatakiwa kujipanga upya kwa ajili ya mechi za kusaka kufuzu kwa Kombe la Dunia, lazima tukubali matokeo," alisema Nyoni.

Naye nahodha msaidizi wa Stars, Aggrey Morris alisema hawana kingine zaidi ya kujiuliza wapi walipokosea ili kurekebisha makosa hayo.

Watanzania wengi waliojitokeza kushuhudia mchezo huo walionyesha kufurahishwa na kiwango cha Stars na kusema hata kama wameondolewa, walicheza kwa kujituma.

Anuary Aziz, Mtanzania anayefanya kazi Maputo alisema hajawahi kuona Watanzania wengi kiasi kile wanaoishi nchini hapa wakijitokeza kushangilia timu yao na kuongeza kuwa walishapata taarifa kuwa Taifa Stars imeboreshwa.

"Kwa kweli timu imebadilika na kocha huyu asisumbuliwe aachwe afanye kazi yake tumeshindwa lakini vijana wamecheza hadi dakika ya mwisho kwa kweli tumefurahi na tumeshangilia sana.

"Tanzania tutafika mbali sana tuwe na subira tu kwani wachezaji wetu wanatupa matumaini sana… mchezo huu ulikuwa wa kwetu lakini tumeshindwa kwa penalti tumekubali matokeo na tunajua tutafika mbali," alisema Mohamed Ali ambaye ni Mtanzania mwingine anayeishi Maputo.

Stars inategemewa kuwasili Jumanne usiku ikitokea Maputo kupitia Nairobi.


Michael Mukunza
Media Manager
Executive Solutions Ltd
P.O. Box 1601, Dar es Salaam
Mobile: 0784/0776/0767978302 or 0714683451

No comments:

Post a Comment