Monday, June 18, 2012

Haas ajishangaa kumfunga Federer fainali

Tommy Haas (kulia) akibeba taji lake la tenisi la  michuano ya Gerry Weber Open baada ya kumfunga Roger Federer (kushoto) katika fainali ya michuano hiyo ya kujiandaa na Wimbledon Open.

NYOTA wa tenisi wa Ujerumani, Tommy Haas amepata ushindi usiotarajiwa dhidi ya bingwa wa mataji 16 ya tenisi ya Grand Slam, Roger Federer na kutwaa ubingwa wa michuano ya Gerry Weber Open mjini Halle.

Federer, ambaye ameshinda mataji matano katika uwanja wa nyasi, alilala 7-6 (7-5) 6-4 katika pambano hilo dhidi ya Haas lilidumu kwa saa 1 na dakika 35.

Mchezaji bora Na.2 wa dunia wa zamani Haas (34), sasa hivi anashikilia Na.87 kwa ubora duniani.
"Kama mtu angesema kabla ya mechi hii kwamba ningemfunga Roger Federer, ambaye bila ya shaka ni mchezaji bora wa zama zote, ningefikiria kwamba wamerukwa na akili," alisema.

Haas alipoteza mechi tisa zilizopita dhidi ya Federer katika kipindi cha miaka 10.

Aliongeza: "Hii imekuwa moja ya wiki bora sana katika maisha yangu ya tenisi lakini sikufikiria hilo hadi jioni hii."

Baada ya Rafael Nadal kufungwa, Federer alipewa nafasi kubwa ya kubeba taji lake la sita la michuano hiyo ya kujiandaa na michuano ya Wimbledon.

Lakini Haas, mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi katika mchezo wa mtu mmoja mmoja, alimbwaga Mswisi Federer kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2002 na kutwaa taji lake la 13 maishani.

No comments:

Post a Comment