Wednesday, June 27, 2012

EUSEBIO AHAMISHIWA HOSPITALI YA URENO

Gwiji wa soka wa timu ya taifa ya Ureno na klabu ya Benfica, Eusebio (kushoto) akizungumza na mkongwe wa taifa hilo Luis Figo wakati wa mechi ya robo fainali ya Euro 2012 baina ya Jamhuri ya Czech na Ureno kwenye Uwanja wa Taifa mjini Warsaw, Poland Juni 21, 2012.

LISBON, Ureno
GWIJI wa zamani wa soka wa timu ya taifa ya Ureno na klabu ya Benfica, Eusebio, alihamishwa kutoka katika hospitali ya Poland na kupelekwa katika chumba cha uangalizi maalum cha hospitalia ya Lisbon jana baada ya kupatwa na matatizo ya moyo wakati akiwa nchini Poland kushuhudia fainali za Euro 2012.

Eusebio, 70, alilazwa katika hospitali ya Luz ya mjini Lisbon baada ya kusafirishwa kwa ndege kurudishwa nyumbani kwa matibabu. Madaktari walisema alikuwa katika hali nzuri.

"Tutapitia kwa kina vipimo alivyofanyiwa nchini Poland. Yuko katika hali nzuri, ya utulivu... tusubiri kidogo, tutatoa taarifa rasmi baadaye," mkurugenzi wa matibabu wa wa hospitali ya Luz, Jose Roquette aliwaambia wanahabari.

"Eusebio alitaka kwenda nyumbani, akisema anajisikia vyema, alikuwa na safari nzuri na hiyo ni dalili njema."

Eusebio, ambaye ni balozi wa soka la Ureno, amelazwa hospitali mara nne tangu Desemba mwaka jana.

No comments:

Post a Comment