Saturday, June 30, 2012

BOLT ASHINDWA NA BLAKE MBIO ZA MITA 100

Usain Bolt (kulia) akimaliza mbio za mita 100 juma ya Yohan Blake (kushoto) wakati wa mbio za kusaka bingwa wa Jamaica za kufuzu kwa Olimpiki 2012 kwenye Uwanja wa Taifa wa Kingston, Jamaica.

USAIN Bolt alipata pigo kubwa katika mbio za mita 100 za timu ya Jamaica za kujiandaa na Olimpiki wakati aliposhindwa na Yohan Blake ambaye aliyetumia muda wa sekunde 9.75.

Blake alimshinda bingwa mtetezi wa Olimpiki Bolt - ambaye alitumia muda wa sekunde 9.86 - na kuweka rekodi ya kasi zaidi kwake na kwa mwaka huu.

Bingwa wa zamani wa dunia wa mbio hizo, Asafa Powell, alimaliza akiwa wa tatu kwa kutumia sekunde 9.88 katika mbio hizo zilizofanyika kwenye Uwanja wa Taifa wa Kingston.

Matokeo hayo yamewafanya wakimbiaji hao wote watatu kufuzu kwa mbio za Olimpiki 2012 zitakazofanyika London.

Muda wa sekunde 9.75 pia unamfanya Blake kuwa mtu wa nne mwenye kasi zaidi kwa wakati wote duniani nyuma ya Bolt anayeshikilia rekodi ya dunia kwa sekunde 9.58, Mmarekani Tyson Gay (sekunde 9.690 na Asafa Powell (sekunde 9.72).

"Sina presha hata kidogo... kila kitu kiko sawa. Nina bahati tu," Blake alisema baada ya kuishinda rekodi yake mwenyewe bora ya sekunde 9.82. "Mimi ndiye bingwa wa taifa la Jamaica kwa sasa, naenda kwenye olimpiki nikiwa hivi."

Bolt baada ya kuondoka taratibu katika mbio zote za nusu fainali na fainali, alisema kuhusu kuanza kwake vibaya: "Ni lazima nipuuze hilo. Nilianza vibaya, lakini nilidumisha ujasiri kwamba sipaswsi kukata tamaa."

Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Bolt na Blake kukutana tangu Blake alipotwaa ubingwa wa dunia mjini Daegu mwaka jana, baada ya bingwa huyo wa Olimpiki kuenguliwa kutokana na kukosea kuanza mbio.

Bolt, ambaye alitwaa medali za dhahabu za Olimpiki za mita 100, mita 200 na za kupokezana vijiti za mita 100x4 kwenye michuano ya Beijing 2008, alikuwa pia akishikilia rekodi ya kukimbia kwa kasi zaidi kwa mwaka huu ya sekunde 9.76 aliyoiweka mjini Rome mwezi uliopita.

No comments:

Post a Comment