Sunday, September 8, 2013

POULSEN: KUKOSEKANA NYOTA KUMETUMALIZA

Beki wa timu ya taifa ya the Gambia , Bubacarr Sanneh akitafuta maarifa ya kuwapita wachezaji wa Stars Khamis Mcha na Erasto Nyoni, katika mchezo wa mwisho wa kuwania tiketi ya kufuzu fainali za Kombe la la Dunia nchini Brazil 2014, mchezo uliofanyika nchini Gambia.

Kocha Kim Poulsen amesema kukosekana kwa wachezaji tisa muhimu ni mojawapo ya sababu ya kushindwa mechi ya Jumamosi na akaiomba TFF kuhakikisha kuwa wachezaji wanaocheza nje wakiitwa wanakuja nyumbani kucheza.

Kocha huyo aliyasema hayo Mjini Banjul mara tu baada ya mchezo na Gambia ambapo wenyeji walishinda kwa bao 2-0 katika mechi ya mwisho ya kuwania kucheza fainali za Kombe la Dunia.

Amesema alikosa wachezaji tisa muhimu amabapo wengine hawakufika kabisa kutoka wanakocheza soka la kulipwa na wengine walikuwa majeruhi.

“Nimeambiwa Gambia waliita wachezaji kumi na moja kutoka nje kwa sababu walitambua umuhimu wa kushinda mechi hii na sisi tulikosa karibu timu nzima,” alisema na kusema ni bora TFF wahakikishe kuwa wachezaji hawa wanapohitajika hasa kwenye mechi za kufuzu kucheza Kombe la Afrika, wanapatikana kwa wakati.

“Tumeijenga hii timu tukiwa na malengo ya kufuzu kucheza fainali hizo za Kombe la Afrika kwa hivyo ni muhimu sana wawepo wanapoitwa,” alisema Poulsen.

Wachezaji wazoefu wa Stars waliokosa mechi hiyo ni, Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu, Kelvin Yondani, Athuman Idd, Salum Abubakar, John Boko, Mwinyi Kazimoto, Shomari Kapombe na Aggrey Morris.

Alisema baadhi ya hawa wachezaji ambao ni vijana, wamejipatia uzoefu mkubwa  pamoja na kwamba walifanya makosa kadhaa uwanjani ambayo anaamini kama wachezaji wenye uzoefu kidogo wangekuwepo wangeweza kudhibiti ile hali kwa nammna moja au nyingine.

Hata hivyo, amesema licha ya timu yake kushindwa na Gambia  hajakata tama kwani malengo aliojiwekea tangu mwanzo ni kufuzu kucheza fainali za Kombe la Afrika 2015, jambo ambalo hata TFF na mdhamini, Kilimanjaro Premium Lager wanalitambua na wanaunga mkono.

Amesema inasikitisha kupoteza mechi lakini watanzania lazima waelewe kuwa malengo ni ya muda mrefu na timu inaendelea kuimarika siku hadi siku.

Alisema huu sio muda wa kulaumu na kukata tamaa kwani safari bado ndefu na tayari kuna dalili nzuri zinaonekeana hasa tangu Taifa Stars ipate udhamini mpya wa Kilimanjaro Premium Lager ambao unawezesha mambo mengi kufanyika sasa kwani imewekeza zaidi ya bilioni 15 kwa miaka mitano.

“Mechi hizi za Kombe la Dunia zimetupa uzoefu kwani Tumeweza kucheza na timu kubwa kama Ivory Coast na Morocco na kuonesha uwezo mkubwa zaidi nah ii inaonesha uwa timu imeimarika kabisa,” alisema.

Kabla ya mechi hiyo baadhi wa wananchi wa Gambia walionesha kutokuwa na imani na timu yao baada ya kutofanya vizuri katika mechi zilizopita.

Geoffrey Kaishozi ambaye ni Mtanzania anaefanya kazi Gambia alisema alifurahishwa na jinsi Stars ilicheza katika kipindi cha kwanza lakini kipindi cha pili mchezo ulibadilika baada ya Gambia  kupata  goli katika dakika ya 45 na lingine katika kipndi cha pili.

“Tumesikitika kuwakosa wachezaji wengi tuliowazoea nap engine kuwepo kwao kungeleta utofauti katika mechi hii,” alisema na kuongeza kuwa ni muhimu wachezaji wale muhimu wawepo katika mechi muhimu kama hizi.

Naye Francis Mushi alisema alienda uwanjani na matumaini kuwa Taifa stars ingeshinda hasa baada ya kuifunga Gambia 2-1 katika mechi ya awali nyumbani.

“Tulicheza vizuri katika kipindi cha kwanza lakini katika kipindi cha pili tulilemewa na tukaamka dakika za mwisho za mpira lkini hatukufanikiwa kupata goli,” alisema na kuongeza kuna umuhimu wa timu kukaa pamoja kwa muda mrefu ili wachezaji waweze kuelewana vizuri uwanjani.

Alisema Gambia pia hawakucheza katika kiwango chao cha kawaida kwa hivyo wengi walitegemea Taifa Stars ingeshinda.

Emmanuel Mtaki ambaye pia anafanya kazi Gambia alisema kulikuwa na makosa mbalimbali kama mabeki kutowadhibiti vizuri washambuliaji wa Gambia, wachezaji wa katikati kutotowa pasi za uhakika ili iwapate washambuliaji na pia nguvu ya ushambuliaji kuwa ndogo.

“Wachezaji wetu lazima wajiamini hata kama wenzao wengne wanakosa, waliopo wajiamini na wafanye kazi uwanjani,” alisema.

Magoli yote ya Gambia katika mchezo wa Jumamosi yalifungwa na nahodha wa timu hiyo Mustafa Jarjue ambaye alicheza mpira wa hali ya juu.

Stars inatarajiwa kuwasili nyumbani Jumatatu saa nane mchana kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya.

No comments:

Post a Comment