Saturday, July 6, 2013

WASANII MWANZA WATAKA MPAMBANO NA KINA JB, RAY TAMASHA LA FILAMU

Wasanii wa Bongo Movie kutoka kushoto Hussein Kambi, JB, Ray, Anti Ezekiel, Irene Uwoya, Chuchu Hans na Jacqueline Wolper wakiwa jukwaani wakati wa uzinduzi wa Tamasha la Filamu kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza
Wasanii wa filamu nchini, Steve Nyerere (kushoto) na Ray wakishambulia jukwaa wakati wa uzinduzi wa Tamasha la Filamu kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza

WASANII mbalimbali wanaojitokeza katika Tamasha la Wazi la Filamu la Grand Malt Tanzania, maarufu kama ‘Grand Malt Tanzania Open Film Festival’ linalofanyika katika Uwanja wa Nyamagana, jijini hapa wamezua mambo kwa kutaka wapambanishwe na wakongwe.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wasanii hao walisema wana uhakika mkubwa wa kuwafunika wakongwe na wanataka mpambano wa ‘live’ siku ya kufunga tamasha hilo hapo kesho.

Akizungumza kwa kujiamini, Paul Mabula ‘Bonge’ alisema msanii Jacob Steven ‘JB’ hawezi kutamba kwake, kwani yeye anajiona ni mkali zaidi kuliko yeye na akikubali wachuane ‘live’ hapo kesho atafanya vitu vya ajabu vitakavyowashangaza wengi.

“Yule JB ni bwa’mdogo tu kwangu, kama anajiamini mwambie Jumapili nipambane naye halafu aone nani mkali, mimi najiamini mno katika kila kitu,” alisema Bonge kwa kujiamini mno.

Isha Rama ambaye mwenyewe anajiita Irene Uwoya, alimtaka msanii huyo pamoja na Jacqueline Wolper wapambane naye, kwani anaweza kuwafunika wote wawili kwa wakati mmoja.

“Nitakuja na dogo wangu hata yeye ana uwezo wa kumfunika (Vicent Kigosi) Ray na watatambua Mwanza kuna vipaji vingi na vyenye uwezo zaidi kuliko wao,” alisema Isha.

Akizungumzia hilo, Meneja wa Grand Malt, Consolata Adam alisema, amefurahi kuona wasanii wa Mwanza wanavyojiamini mno na kuwatahadharisha wakongwe wakae chonjo kesho kwa upinzani mkubwa watakaoupata.

“Hapa Mwanza tumeshuhudia vipaji vya kila aina, nimefurahi kwa kiasi kikubwa kwa jinsi wanavyojiamini, kwetu Grand Malt tunaamini lengo letu limefanikiwa kwa kiasi kikubwa,” alisema.

Mratibu wa Tamasha hilo, Musa Kissoky, alisema naye amefurahishwa pia na wazo la wasanii hao na kuwaonya wakongwe watakutana na vitu visivyo vya kawaida hiyo kesho.

“Hapa Mwanza kuna balaa tupu, maana hawa wasanii sikutegemea kama wanajiamini kwa kiasi kikubwa kama hivi, tutaona hiyo Jumapili mambo yatakavyokuwa,” alisema.

Tamasha la Filamu la Grand Malt lilianza rasmi mwishoni mwa wiki na linatarajiwa kumalizika kesho, huku wakati wote wa tamasha hilo zikionyeshwa filamu mbalimbali za Tanzania.

Tamasha hilo la filamu limedhaminiwa na kinywaji cha Grand Malt kisicho na kilevi ambacho kinazalishwa na kusambazwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).

No comments:

Post a Comment