Wednesday, July 24, 2013

IBRA: SINA SABABU YA KUONDOKA PSG

Ibrahimovic

PARIS, Ufaransa
ZLATAN Ibrahimovic amekanusha uvumi kwamba ataondoka PSG baada ya klabu hiyo kumsajili mshambuliaji Edinson Cavani kwa ada ya uhamisho ya paundi milioni 54 kutoka Napoli.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 31 alifunga magoli 30 na kutoa pasi za magoli 10 katika mechi 34 za ligi katika msimu wake wa kwanza klabuni hapo msimu uliopita, na kuiongoza timu hiyo kutwaa ubingwa akiwa mfungaji bora wa Ligue 1.

Hata hivyo, uvumi uliendelea kuzagaa kwamba mchezaji huyo wa kimataifa wa Sweden yuko mbioni kuhama kufuatia kusajiliwa kwa Cavani, lakini Ibrahimovic amesema hajawahi kufikiria kuondoka katika kikosi hicho cha kocha Laurent Blanc.

“Sina sababu ya kuondoka,” aliwaambia waandishi wa habari.
“Nachezea PSG na sijawahi kufikiria kuondoka. Nitazungumza na klabu, lakini hakuna cha muhimu cha kukisema.

“Uvumi huu huja kila kipindi cha usajili. Vyombo vya habari vishanisajili katika klabu zote za Ulaya.

“Nina mkataba na PSG, lakini bado sijakutana na rais. Bado nina miaka miwili katika mkataba wangu, na kwa kuwa mimi ni mweledi, nilienda kuwaona."

Ibrahimovic haoni nafasi yake ikiwa hatarini kufuatia kununuliwa kwa mshambuliaji huyo wa Uruguay na anafuraha kumkaribisha Paris, pamoja na kocha mpya Blanc.

“Sijawahi kucheza na Cavani hapo kabla. Kama ilivyo kwa mchezaji yeyote ni lazima uzoee mazingira. Ni lazima ajifunze kuhusu timu na klabu na mji. Atakuwa na mchango muhimu kwa timu yetu," aliendelea.

“Nilimfahamu Blanc kabla hajaja klabuni hapa. Nilikutana naye katika fainali zilizopita za Mataifa ya Ulaya (Euro) 2012 na mara nyingine kadhaa. Klabu ni mpya kwake na mimi, na wengine wote ni lazima tujiandae kwa msimu ujao. Tunahitaji kufahamiana. Hatuna cha kupoteza. Nina hakika atafanikiwa Paris."

PSG, ambayo imemwaga paundi milioni 97 katika kuwasajili Lucas Digne, Marquinhos na Cavani katika wiki moja iliyopita, wamefunikwa na timu iliyopanda daraja ya Monaco.

Klabu hiyo ya Monaco imetumia paundi milioni 126 katika kusajili wachezaji wapya sita, akiwamo Radamel Falcao, James Rodriguez na Joao Moutinho katika kipindi hiki cha usajili, lakini Ibrahimovic bado anaiamini timu yake.

Aliongeza: “Hakika naiona Monaco kama wapinzani wakubwa. Wana mpango mkubwa. Tofauti ni kwamba sisi tuna faida ya uzoefu mwaka mmoja ama miwili.

“Nawaachia wengine wazungumze wanaponilinganisha na Falcao. Kitu muhimu kwangu ni kuisaidia timu ishinde. Napenda kuwaachia wengine wazungumze."

No comments:

Post a Comment