Monday, June 24, 2013
VODACOM KUKABIDHI ZAWADI LIGI KUU BARA JULAI 3
WADHAMINI wakuu wa Ligi Kuu ya soka ya Tanzania Bara Kampuni ya Vodacom imetangaza kuwa itakabidhi zawadi kwa washindi wa ligi hiyo Julai 3 jijini Dar es salaam.
Vodacom imesema ilikuwa ikisubiri kumalizika kwa hekaheka za timu ya taifa - Taifa Stars za kusaka nafasi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil hali iliyochelewesha tukio la kukabidhi zawadi hizo kwa mabingwa pamoja na wote waliofanya vema katika msimu wa 2012/2013.
.
"Tulikuwa tukisubiri wakati mwafaka wa kufanya hivyo kwani tangu kumalizika kwa ligi mwezi uliopita mwelekeo wa taifa ulikuwa ni kuipa ari na nguvu timu yetu ya taifa katika kusaka tiketi ya kufuzu kushiriki fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil," alisema Meneja Uhusiano wa Nje wa Vodacom Salum Mwalim.
Mwalim amesema maandalizi yote ya tukio hilo yamekamilika kwani hakukuwa na sababu nyingine ya kutokabidhi zawadi mara tu baada ya ligi kumalizika zaidi ya timu ya taifa - Taifa Stars.
Mwalim amesema hafla ya utoaji wa zawadi inahitaji ushiriki wa wadau mbalimbali wa soka nchini wakiwamo wachezaji wa klabu ambao miongoni mwao wamo kwenye kikosi cha Stars, viongozi wa TFF na walimu wa timu ya taifa ambao wote hao kwa pamoja walikuwa na jukumu moja tu la kuhakikisha Stars inafuzu kwenda Brazil na hivyo isingekuwa vema kuingiza maandalizi ya jambo jingine katikati ya juhudi hizo.
Mwalim ametumia nafasi hiyo kuzishukuru klabu pamoja na Shirikisho la Soka (TFF) na kamati ya ligi kwa uvumulivu wao wakati wote ambapo Vodacom ilikuwa ikisubiri kupatikana kwa muda mwafaka wa kukabidhi zawadi.
"Tendo la kukabidhiwa zawadi ni moja ya matendo makuu kabisa kwa yeyote anayeshinda, tumeona uvumilivu mkubwa na wenzetu walituelewa wakati tulipowashauri kutoa nafasi kwa Stars bila kuharibu concentration ya taifa. Tumeonesha umoja wetu."
Vodacom itakabidhi zawadi za fedha taslimu takribani Sh. milioni 200 kwa mabingwa Yanga na Azam, Simba na Kagera Sugar zilizoshika nafasi ya pili hadi ya nne.
Mbali ya mabingwa timu ya Yanga ambayo itakabidhiwa fedha taslimu Sh milioni 70, wengine watakaotunukiwa ni wachezaji mmoja mmoja walioonesha umahiri kwenye maeneo yao.
Wengine watakaonufaika na zawadi za fedha ni kipa bora, mwamuzi bora, mwalimu bora, timu iliyoonyesha nidhamu na mfungaji bora, ambaye ni Kipre Tchetche wa Azam.
Vodacom imekuwa ikiidhamini ligi kuu ya soka ya Tanzania bara kwa zaidi ya misimu mitano sasa huku ikiiwezesha ligi hiyo kuimarika na kuwa ya ushindani kadri miaka inavyosonga mbele.
Labels:
Michezo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment