Wayne Rooney... njiani Arsenal? |
MKURUGENZI Mtendaji wa Arsenal, Ivan Gazidis amechochea uvumi unaomhusisha Wayne Rooney na uhamisho wa kutua Emirates Stadium, baada ya kubainisha kwamba The Gunners wanao uwezo wa kifedha wa kumvutia mshambuliaji wa Manchester Unitedm Wayne Rooney (27).
Kocha Arsene Wenger tayari alishabainisha kwamba itakuwa ni vigumu kutotangaza ofa ya kumsajili mshambuliaji huyo kama atakuwa sokoni, huku ikiaminika kwamba Rooney yuko tayari kutua Arsenal.
Na sasa Gazidis amechochea uvumi kwamba Arsenal wanaendelea na mipango ya kumsajili nyota huyo wa timu ya taifa ya England, akisema kwamba gharama za uhamisho na mshahara wa Rooney vyote viko ndani ya bajeti ya Arsenal.
Alipoulizwa kama Arsenal watamudu gharama zinazozidi paundi milioni 20 za ada ya uhamisho na mshahara wa paundi 200,000 kwa wiki, Gazidis aliwaambia waandishi wa habari: "Hakika tunamudu. Tunamudu zaidi ya hapo.
"Tuna pesa ambazo tuliziweka akiba. Pia tuna njia nyingine za mapato na yote haya yanamaanisha kwamba tunaweza kufanya mambo ambayo yatawashangazeni.
"Kama Arsene anadhani kwamba kusajili majina makubwa ni jambo sahihi la kufanya, sawa. Ukweli ni kwamba mwaka huu tunaanza kushuhudia mambo ambayo tumekuwa tukiyapanga kwa muda mrefu, ambayo ni kukua kwa uwezo wetu kifedha.
"Tunaweza kuanza kuangalia machaguo ambayo hayakuwa katika uwezo wetu kifedha. Ni mabadiliko ya katika miaka miwili ijayo. Ni muhimu kwa klabu."
Licha ya Gazidis kukataa kutaja wachezaji wowote wanaowawania, anaamini kwamba malengo ya Arsenal yanaweza kuwashuhudia wakisajili kama mabingwa wa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, Bayern Munich.
"Tunataka kushindana katika matawi ya juu kama Bayern Munich. Sisemi kwamba tutalazimisha kufika pale kwa namna yoyote, tuko mbali nyuma kabla hatujajiweka katika matawi yale," Gazidis aliendelea. "Nadhani sisi ni klabu yenye malengo makubwa mno.
"Safari hii yote kwa miaka 10 iliyopita ilikuwa ni kujaribu kujiweka katika daraja moja na klabu bora duniani na sasa swali ni kuyageuza mafanikio hayo kuwa mafanikio ya uwanjani."
No comments:
Post a Comment