Saturday, June 8, 2013

PRISCA AMVUA TAJI LA SINZA MISS TANZANIA BRIGITTE ALFRED

Redd's Miss Sinza 2013, Prisca Element (katikati) akiwa na Mshindi wa pili Happynes Maira (kulia) na Mshindi wa tatu, Sarah Paul, baada ya kutangazwa washindi katika shindano lao lililokuwa likishikiliwa na Redd's Miss Sinza na Miss Tanzania 2012-2013, Brigitte Alfred
Miss Sinza 2012-2013, Brigitte Alfred (kushoto) akimvisha taji mrithi wake Redd's Miss Sinza 2013, Prisca Element, baada ya kutangazwa mshindi wa shindano hilo lililofanyika usiku wa kuamkia leo kwenye Ukumbi wa Meeda Club, Sinza jijini Dar es Salaam.


PRISCA Element usiku wa kuamkia jana, alitwaa taji la Redds Miss Sinza 2013 katika kinyang'anyiro kilichowashirikisha jumla ya warembo 12, kwenye ukumbi wa Meeda Club na kurithi taji la kwanza la Redds Miss Tanzania, Brigitte Alfred.

Haikuwa kazi rahisi kwa Prisca kutwaa taji hilo kutokana na ushindani mkubwa kutoka kwa warembo bora 11 walioshiriki mashindano hayo yaliyodhaminiwa na Redds Original, Dodoma Wine, Fredito Entertainment, Chilly Willy Energy Drink, Sufiani Mafoto blog, Salut5 na CXC Africa.

Hata hivyo, Prisca aliweza kuwazidi kete wanzake na kutwaa taji hilo sambamba na zawadi ya Kitita cha Sh. 400,000 zilizotolewa na waandaaji wa mashindano hayo  Calapy Entertainment chini ya ukurugenzi wa Majuto Omary.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Sinza A, Juma Mgendwa alikabidhi zawadi hiyo kwa Prisca ambaye alisema kuwa amefurahi kushinda taji hilo na kazi yake kubwa ni kutwaa taji la Miss Kinondoni.

"Kwangu ni historia kutokana na ukweli kuwa nimerithi taji la Redds Miss Tanzania Brigitte Alfred, na ninaahidi kufanya kweli katika mashindano yanayofuata na kutwaa mataji ya Miss Kinondoni na vile vile taji la Redds Miss Tanzania, nitashirikiana na waandaji wangu ili kufanya maandalizi ya kina ili kufikia malengo hayo," alisema Prisca.

Nafasi ya pili ilichukuliwa na Happiness Maira ambaye alizawadiwa sh. 300,000 alizokabidhiwa na Mratibu wa Masoko na Biashara wa kinywaji cha Dodoma Wine, Frank Matonda na zawadi ya mshindi wa tatu ilikwenda kwa Sarahy Paul na kukabidhiwa zawadi ya shs 200,000 na Swabir Abdulrehman ambaye ni Mkurugenzi wa Usambazi wa Kampuni ya TSN Distribution kupitia kinywaji cha Chilly Willy.

Nafasi ya nne ilichukuliwa na Nicole Michael na tano ilichukuliwa na Nasra Hassan ambao wote walizawadiwa shs 150,000 kila mmoja na  Mkurugenzi wa Mashindano hayo, Majuto. Warembo hao watano wataiwakilisha Sinza katika mashindano ya Miss Kinondoni 2013.

Mashindano hayo yalishuhudiwa na umati mkubwa wa mashabiki wa urembo na kupambwa na burudani safi ya bendi bora nchini, African Stars maarufu kwa jina la Twanga Pepeta ambayo ilitambulisha baadhi ya nyimbo zake mpya za albamu ya Nyumbani ni Nyumbani.Twanga Pepeta ilifanya mambo makubwa jukwaani huku ikiwa ikitumbuiza kwa mara ya kwanza kwa kipindi cha mwaka mmoja na zaidi.

No comments:

Post a Comment