Friday, June 7, 2013

TAIFA STARS SASA IMEJITOSHELEZA - TENGA

Leodegar Tenga

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeishukuru Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa kuiwezesha timu ya taifa, Taifa Stars kuondokana na matatizo na kuwaomba Watanzania kuiombea timu ili ifanye vizuri katika mechi yake ya leo dhidi ya Morocco mjini Marrakech.

Stars, ambayo inashika nafasi ya pili kwenye kundi lake la mashindano ya awali ya Kombe la Dunia ikiwa nyuma ya Ivory Coast kwa tofauti ya pointi moja, leo inacheza dhidi ya Morocco katika mechi ya nne itakayofanyika mjini Marrakech baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 katika mechi ya kwanza iliyofanyika Dar es salaam mwezi Machi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, rais wa TFF, Leodegar Tenga alisema kuwa tangu kuanza kwa udhamini, TFF haijawahi kupata udhamini mkubwa kama wa Kilimanjaro Premium Lager ambayo imeingia mkataba wa miaka mitano wa kuidhamini Stars wenye thamani ya dola milioni 10 za Marekani.

“Katika kipindi chote hiki hatujawahi kupata udhamini ambao umekidhi mahitaji yote ya timu kama huu wa TBL,” alisema Tenga kwenye mkutano na waandishi uliofanyika kwenye ofisi za TFF. “Lakini katika mwaka mmoja uliopita (tangu TBL ianze kudhamini) hatujawahi kushindwa kuisafirisha timu; kushindwa kulipa posho za wachezaji; kutanguliza watu wetu kwenda nje kuiandalia timu sehemu nzuri; kuzilipia tiketi za ndege timu tunazocheza nazo mechi za kirafiki na hata kuzilipia ada ya kucheza mechi.

“Posho za wachezaji zimepanda kwa karibu mara mbili na ndio maana leo wachezaji wanaijali timu yao. Yote haya ni kutokana na udhamini huu. Watu wanasema usione vinaelea….”

Tenga alisema kuwa udhamini huo ndio sasa umeanza kuzaa matunda na timu inafanya vizuri ikiwa ni pamoja na kuwa na maandalizi ya muda mrefu.

“Sasa tunawaomba Watanzania waiombee timu na tunawashukuru wale waliokwenda Morocco kuishangilia timu kwa kuwa vijana wetu wanapata nguvu pale wanapoona kuna watu wako nyuma yao,” alisema Tenga.

Rais huyo wa TFF pia alisifu kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kuiita timu Ikulu na kuongea na kula na wachezaji, akisema kitendo hicho kitasaidia kuongeza hamasa kwenye timu.

Naye Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe alisema kampuni yake itaendelea kuwa bega kwa bega na TFF na kwamba uhusiano baina ya pande hizo mbili umeimarika na utaendelea kuimarika.

Katika mkutano huo, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Tanzania (NSSF) ulikabidhi fulana maalum kwa ajili ya mashabiki ambao wamekwenda Morocco kuishangilia timu. Afisa Uhusiano Mwandamizi wa NSSF, uma Kintu alisema tayari fulana 250 zimegawiwa kwa mashabiki walioko Morocco na nyingine zilitarajiwa kusafirishwa jana.
 

No comments:

Post a Comment